2015-11-28 16:59:00

Nyumba ya upendo Nalukolongo Bakateyamba ni ushuhuda wa Injili ya uhai


Askofu Robert Muhiirwa  mwenyekiti wa Tume ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda anasema, Nyumba ya Upendo ya Nalukolongo imejengwa mahali ambapo kwa mara ya kwanza, katekesi ilitolewa kwa watu waliokuwa wanajiandaa kupokea Sakramenti ya Ubatizo. Nyumba hii ni kielelezo cha upendo kwa Mungu na jirani. Ni nyumba inayotoa huduma pasi na upendeleo wala ubaguzi kwa mtu awaye yote.

Nyumba ya upendo ilianzishwa kunako mwaka 1978 na kwa sasa inatoa huduma kwa walemavu na wazee wapatao 102. Watu wanaohudumia hapa wanatoka Uganda, Tanzania, Kenya, DRC, Rwanda, Burundi na Sudan ya Kusini. Kuna walemavu ambao wamekuwepo nyumbani hapa wakihudumiwa kwa takribani miaka 20 hadi miaka 28. Kijana mdogo kuliko wote ana umri wa miaka 11 na mzee wa wote ana umri wa miaka 107, matendo makuu ya Mungu!

Mkutano huu umehudhuriwa pia na Madaktari, waguzi na wahudumu wa kutoka katika sekta ya afya wanaofanya kazi katika Majimbo 19 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Uganda. Kanisa linamiliki vituo vya afya 288 sehemu mbali mbali za Uganda. Mkutano huu pia umehudhuriwa na wafanyakazi kutoka sekta ya afya Serikalini na mashirika ya kujitegemea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.