2015-11-28 09:17:00

Makatekista wanamshukuru na kumpongeza Papa Francisko kwa kuwaona!


Familia ya Mungu nchini Uganda, Ijumaa jioni tarehe 27 Novemba 2015 imepokea Baba Mtakatifu Francisko alipowasili kwenye eneo la Munyonyo kwa mishumaa iliyokuwa inawaka, kielelezo cha moto wa imani uliowashwa na Roho Mtakatifu wakati mashuhuda wa imani walipobatizwa. Baba Mtakatifu amebahatika kubariki jiwe la msingi lililotolewa kwenye Kaburi la Mtakatifu Francisko wa Assisi nchini Italia kama kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mashahidi wa Uganda walipotangazwa kuwa Watakatifu.

Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na Makatekista na walimu wa dini shuleni ili kutambua mchango na dhamana ya Makatekista katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna zaidi ya Makatekista 14, 000 wanaohudumia Familia ya Mungu nchini Uganda na kwamba, wao wako chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Andrea Kaggwa, shuhuda wa imani; kijana aliyebahatika kufunga Ndoa Takatifu na asali wa moyo wake Batudde Nakazibwe ambaye baada ya ubatizo wake alipewa jina jipya Klara. Hii ni ndoa ya kwanza kufungwa nchini Uganda, ikawa ni mfano wa kuigwa na wengi. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Uganda kutangaza na kushuhudia Injili ya familia ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi kama walivyokaza kusema Mababa wa Sinodi ya familia iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepanda mti kielelezo cha ushuhuda wa Uekumene wa damu unaopania pamoja na mambo mengine kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kukuza na kudumisha utamaduni wa kutunza mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu pia amebariki Sanamu ya Mtakatifu Andrea Kaggwa pamoja na kupitia eneo alipouwawa Mtakatifu Denis Ssebugwawo aliyekuwa na umri wa miaka 16 tu alipokumbana na mkono wa chuma wa Mfalme Mwanga.

Askofu mkuu Cyprina Kizito Lwanga alipembua kwa kina na mapana maana ya eneo la Munyonyo katika maisha na utume wa Kanisa nchini Uganda kuwa ni mwanzo wa safari ya ushuhuda wa imani uliohitimishwa Namgongo kwa waamini 22 kutoka Uganda kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake na kutangazwa kuwa Watakatifu wakati wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hii ni changamoto kwa Wakristo kuchuchumilia mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo Yesu, mchungaji mkuu. Huu ni mwendelezo wa umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kujenga umoja wa Kanisa.

Kwa upande wake, Katekista Matia Mulumba Ssemakula, Mratibu wa Makatekista nchini Uganda, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwapatia upendeleo na heshima ya pekee wakati wa hija yake Barani Afrika. Kuna umati mkubwa wa Makatekista wanaojisadaka kila siku kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake chini ya usimamizi na uongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda wanaotoa malezi na majiundo endelevu ili kuhakikisha kwamba, kweli Makatekista wanatekeleza kazi hii takatifu kwa ari na moyo mkuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.