2015-11-28 07:02:00

Makatekista ninyi ni "majembe mazito" yanayofanya kazi takatifu!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuwasili Entebbe, Uganda Ijumaa tarehe 27 Novemba 2015 alipata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanasiasa pamoja na wanadiplomasia nchini Uganda. Baba Mtakatifu amekazia mchango wa mashuhuda wa imani kama mashujaa wa nchi; umuhimu wa Bara la Afrika katika medani mbali mbali za kimataifa pamoja na kuishukuru Uganda kwa kuwakarimu wakimbizi na wahamiaji.

Baadaye, Baba Mtakatifu jioni alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Makatekista pamoja  na waalimu kutoka Uganda huko Munyonyo, mahali ambapo maamuzi ya mauaji ya mashuhuda wa kwanza wa imani nchini Uganda yalifanyika kwa kuwaambia kwamba, wao ni “majembe mazito yanayofanya kazi takatifu; wanaalikwa kuwa kweli ni mashuhuda wa utakatifu wa maishana kwa kutoka kimasomaso bila woga ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Makatekista wameteuliwa kwa ajili ya huduma ya Katekesi, muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Kumbe, Makatekista ni sehemu muhimu sana ya wahudumu wa Kanisa wanaochangamotishwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu katika kila kijiji na kitongoji nchini Uganda. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu, daima wakiwa karibu na Familia ya Mungu nchini Uganda katika uhalisia wa maisha yake, ili kukuza na kuboresha imani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata pale dhamana hii itakapoonekana kuwa nzito kutokana na upungufu wa rasilimali na vitendea kazi; watakapokabiliana na vikwazo pamoja na kinzani za maisha, watambue kwamba, kazi yao ni takatifu na kwamba Roho Mtakatifu yuko na anatenda pamoja nao wakati wote wanapomtangaza Kristo Yesu na kwamba, Roho Mtakatifu atawakirimia mwanga na nguvu wanazohitaji katika utekelezaji wa utume wao! Katekesi kwa vijana na watoto ni muhimu sana katika mchakato wa kurithisha imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo. Makatekista wanapaswa kuwa kweli ni walimu na mashuhuda wa imani tendaji!

Baba Mtakatifu anawakumbusha Makatekista na walimu kwamba,  imani ya Kikristo nchini Uganda imekuwa na kuboreka zaidi kutokana na ushuhuda uliotolewa na Mashahidi wa Uganda waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa; maamuzi yaliyotolewa na Mfalme Mwanga katika eneo la Munyonyo. Hapa mashuhuda wa kwanza wa imani wakachomwa moto na Jamii ya Uganda ikashuhudia Andrea Kaggwa na wenzake wakiwa wamesimama kidete kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, huku wakiambata ahadi za Kristo!

Baba Mtakatifu anamwomba Mtakatifu Andrea, msimamizi wa Makatekista Uganda kuwaombea ili kweli Makatekista nchini humo waweze kuwa walimu wenye hekima, wanaoshuhudia kwa maneno na matendo ukweli angavu wa Mungu na furaha ya Injili. Wawe ni mashuhuda wa utakatifu wa maisha, kwa kutoka kimasomaso kutangaza na kueneza mbegu ya Neno la Mungu; wawe na imani kwa ahadi ambazo Kristo ametoa kwa wafuasi wake, kwani watarejea kutoka katika utume wao wakiwa na kicheko cha furaha midomoni mwao na mavuno mengi. Baba Mtakatifu anawaomba Makatekista na waalimu kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.