2015-11-27 16:19:00

Ujumbe wa Watanzania uko Uganda kushiriki mapokezi ya Papa Francisko


Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora na Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anaongoza ujumbe wa Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania nchini Uganda ili kukutana na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu anapotembelea Uganda, ili kuwaimaarisha ndugu zake katika imani, tayari kujisadaka kwa ajili ustawi na maendeleo ya wengi. Huu ni mwaliko wa kutoka kifua mbele tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya imani tendaji!

Haya yamesemwa na Padre Raymond Saba, Katibu  mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Mabus mawili yaliyobeba waamini kutoka Tanzania yaliondoka Jijini Mwanza siku ya Alhamisi kuelekea Namgongo Uganda, tayari kuungana na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, hapo ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumamosi, tarehe 28 Novemba na kabla ya hapo atatembelea Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda kutoka Kanisa Anglikana, lengo ni kuhamasisha Uekumene wa damu miongoni mwa Wakristo.

Padre Raymond Saba kwa namna ya pekee kabisa anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufuatilia hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kwani ujumbe wake ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ni ujumbe unaojikita katika misingi ya haki, amani na upatanisho mambo mazito katika kukoleza mafungamano ya kijamii. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Uganda na Kenya yalitoa mwaliko kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ili kushiriki katika hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika, Tanzania ikaamua kwenda Uganda, ili kushiriki Ibada ya Misa Takatifu, tayari kuanza mchakato wa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, ili kutangaza Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa sanjari na kuangalia mahitaji ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na mwandishi maalum kutoka Dar Es Salaam.

Imehaririwa na Pd. Richard A. Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.