2015-11-27 10:31:00

Ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Uganda ni tukio la neema!


Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Uganda imebahatika kutembelewa na Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1969 na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1993. Mwenyeheri Paulo VI alitembelea Uganda ili kutoa heshima zake kwa mashuhuda wa imani 22 walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Alisema kwamba, mashuhuda wa imani ni watu ambao wamelipatia heshima kubwa Bara la Afrika, kielelezo makini cha upendo na huruma ya Mungu inayofumbatwa kwenye Fumbo la Msalaba.

Aliwataka watu kuheshimu na kuthamini mila na desturi njema za kiafrika pamoja na kutoa changamoto kwa Waafrika kuwa wamissionari miongoni mwa Waafrika wenzao, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa Watu wa Mataifa kwa kujikita katika majiundo makini kwa waamini walei pamoja na kuendelea kushuhudia umoja na mshikamano wa Kanisa Katoliki.

Hija ya Mwenyeheri Paulo VI lilikuwa ni tukio la neema na baraka kubwa kwa Kanisa Barani Afrika, kwani akiwa nchini Uganda aliwawekwa wakfu Maaskofu 12, tayari kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili pamoja kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Hiki pia kilikuwa ni kipindi cha vugu vugu la kutafuta uhuru Barani Afrika, Mwenyeheri Paulo VI akawatia shime ya kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wao. Alilitaka Kanisa kushiriki kikamilifu katika majiundo ya jamii inayowajibika barabara kwa kutengeneza pia miundo mbinu itakayojikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kanisa lilipaswa kutekeleza dhamana hii kwa kuzingatia imani na upendo kwa watu bila kuwa na ubaguzi, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwenyeheri Paulo VI alikazia kwa namna ya pekee kabisa masuala ya: haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mashahidi wa Uganda wawe ni mbegu ya amani, changamoto kwa waamini walei kufuata nyayo zao kwa kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha, tayari kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya kila siku.

Inapendeza sana kuwa Mkristo, lakini si rahisi sana kuwa Mkristo mwema na mtakatifu, hapa yataka moyo, ujasiri, upendo, sadaka na udumifu.Mashuhuda wa imani nchini Uganda ni kielelezo cha mshikamano wa imani na umoja wa kitaifa na kwamba, mashuhuda wa Uganda ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Kanisa lake. Haya ni maneno ambayo yanapaswa kuacha chapa ya kudumu katika akili na mioyo ya watu!

Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Uganda kunako mwaka 1993 aliwataka Waganda kuachana na tofauti zao zilizopelekea vita na kinzani za kijamii na kuanza mchakato wa ujenzi wa Uganda mpya inayojikita katika: haki, amani, upatanisho, umoja na mshikamano wa kitaifa, tayari kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Uganda; utu na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Hii ni changamoto ambayo bado inapaswa kufanyiwa kazi kwa ari na moyo mkuu nchini Uganda kwani hadi leo hii, bado Waganda wamegawanyika!

Papa Yohane Paulo II aliwataka waamini kwa namna ya pekee, kuhakikisha kwamba wanafuata kikamilifu nyayo za mashuhuda wa imani, ili kujenga Kanisa Katoliki linalojitamadunisha, ili kuzamisha mizizi yake katika mila na desturi njema za Kiafrika. Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, inapaswa kujionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya utii kwa Injili na Mafundisho ya Kanisa na kwamba, Waganda wanapaswa kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa. Mambo haya yajioneshe kwa namna ya pekee katika wema, haki na ukweli ili kujiondoa katika utamaduni wa kifo, ili kushuhudia nguvu ya Msalaba wa Kristo, chemchemi ya upendo, huruma, amani na upatanisho wa kweli.

Jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda, kudumisha na kutetea utu na heshima ya binadamu, ili kujenga amani na utulivu katika medani mbali mbali za maisha. Waganda wenyewe wawe ni vyombo na wajenzi wa Injili ya amani! Dhana ya utamadunisho inapaswa kujikita katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi!

Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki anasema Mtakatifu Yohane Paulo II, ni muhtasari wa Imani, Sakramenti, Maisha adili na Sala; mambo yanayopaswa kufundishwa kwa waamini hatua kwa hatua katika maisha yao ya Kikristo sanjari na kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hii inatokana na ukweli kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, ukarimu na msamaha.

Vijana wajengewe uwezo ili kuwa tayari kutoka kimasomaso kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kati ya ndugu zao. Waganda wanapaswa kuwa ni wajenzi wa nchi yao na kwamba, Kanisa Katoliki lisaidie kwa hali na mali katika mchakato huo kwa njia ya huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu! Kanisa linahitaji uhuru wa kuweza kutekeleza dhamana na utume wake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Uganda na wala halihitaji upendeleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.