2015-11-24 10:17:00

Maandamano ya amani yako njiani kuelekea Nairobi!


Msafara wa mahujaji wa amani kutoka Jimbo kuu la Mombasa, Jumanne tarehe 24 Novemba 2015 mapema asubuhi umeondoka Mombasa kuelekea Nairobi, ili kumpokea Baba Mtakatifu Francisko anayetarajiwa kuwasili nchini Kenya, Jumatano jioni, tayari kuanza hija yake ya kitume kwa mara ya kwanza Barani Afrika. Hawa ni mahujaji wa amani, wanaopenda kujikita katika mchakato wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu; uchumi unaojikita katika haki; majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi pamoja na amani na utulivu mambo msingi katika mchakato wa ustawi wa watu!

Maandamano ya amani yana mwelekeo wake kama mkutano wa wakuu wa dini mbali mbali ulioitishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II mjini Assisi ili kuombea amani na utulivu sehemu mbali mbali za dunia. Maandamano haya yanawashirikisha waamini wa dini mbali mbali kutoka Mombasa, ili kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuvuka kinzani na misigano ya kidini ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa maisha ya watu na mali zao.

Kwa miaka mingi, Kenya imejikuta ikitumbukizwa katika giza na wasi wasi kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Somali, hali ambayo imeunda pia makundi ya kigaidi na waamini wenye misimamo mikali ya kidini, hali ambayo imedhohofisha mafungamano ya kijamii nchini Kenya kwa misingi ya udini na hata wakati mwingine ukabila. Wazo la kuwa na maandamano ya amani kutoka Mombasa ni liliibuliwa na Licio D’Avossa kutoka Cremona, Italia kwa kushirikiana na Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde.

Lengo ni kuwahamasisha wananchi wote wa Kenya kutambua kwamba, ulinzi na usalama uko mikononi mwao wenyewe na kamwe wasiruhusu watu wachache kuharibu misingi ya haki, amani na utulivu nchini mwao kwa mafao ya binafsi. Ubaguzi na kinzani za kidini ni mambo ambayo kwa sasa yamepitwa na wakati na wananchi wote wa Kenya wanapaswa kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.