2015-11-24 09:50:00

Familia ya Mungu nchini Uganda ina matumaini kwa ujio wa Papa Francisko


Askofu Giuseppe Franzelli wa Jimbo Katoliki Lira, Uganda katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Familia ya Mungu nchini Uganda inapenda kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili atakapowasili Entebe, Uganda, Ijumaa tarehe 27 Novemba 2015 na kuondoka nchini humo tarehe 30 Novemba 2015 tayari kuelekea Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ili kufungua lango la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Familia ya Mungu nchini Uganda inapenda kumwonesha Baba Mtakatifu Francisko upendo na mshikamano kwa kuwapatia heshima ya kuwatembelea anapokwenda nchini Uganda kutoa heshima zake za dhati kwa Mashahidi wa Uganda waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, yapata miaka 50 iliyopita. Hii ni nchi ya pekee ambayo imetembelewa na Mapapa watatu: Mwenyeheri Paulo VI, Mtakatifu Yohane Paulo II na Sasa Baba Mtakatifu Francisko.

Familia ya Mungu nchini Uganda inatambua kwamba, hija hii ni ya kitume, Baba Mtakatifu anakwenda nchini Uganda ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa imani tendaji kama ilivyokuwa kwa Mashahidi 22 wa Uganda. Waamini wanapaswa kuwa imara katika imani pasi na wasi wasi wala makunyanzi, changamoto kubwa na endelevu hasa nyakati hizi ambazo kuna mmong’onyoko mkubwa wa maadili na utu wema; kuna tabia ya watu kutaka kukengeuka na kumwondoa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyao. Baba Mtakatifu anakuja ili kuliimarisha Kanisa Katoliki nchini Uganda, ili liendelee kuwa kweli ni sautu ya Kinabii.

Uganda hivi karibuni imesherehekea kumbu kumbu ya miaka 53 ya uhuru wake kwa kuangalia historia, mafanikio pamoja na changamoto nyingi zilizoko mbele yao anasema Askofu Giuseppe Franzelli. Bado kuna haja ya kujita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho kwani Kaskazini mwa Uganda, watu wengi wameguswa na athari za vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa takribani miaka 20, vita ambayo imekuwa ikiendeshwa na Joseph Kony. Haya ni madonda yanayohitaji uponyaji wa ndani, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu.

Uganda bado imegawanyika kisiasa na kikabila; mambo ambayo yanakwamisha mchakato wa umoja na mshikamano wa kitaifa, hasa wakati huu, vyama vya kisiasa vinapoendelea na kampeni zake, tayari kushiriki kwenye uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari 2016. Kumbe, Baba Mtakatifu anakuja kuwaimarisha Waganda kujikita katika upatanisho na umoja wa Kitaifa kwa kuendeleza amana iliyoachwa na Mashahidi wa Uganda, kielelezo cha ushuhuda wa imani unaojikita katika damu ya mashahidi.

Miongoni mwa Mashahidi wa Uganda kuna Makatekista, nafasi ya kuwaenzi na kuwaunga mkono Makatekista katika maisha na utume wao Barani Afrika. Mababa wa Kanisa daima wanasema, damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo! Kanisa nchini Uganda linaendelea kushamiri kutokana na damu ya mashuhuda wa imani. Kuna idadi kubwa ya waamini wa Kanisa Katoliki na kwamba, vyama vya kitume viko moto moto katika utekelezaji wa maisha na utume wa Kanisa nchini Uganda.

Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, waamini wanafundwa barabara ili kuifahamu: Imani wanayoungama; Imani wanayoiadhimisha katika Sakramenti za Kanisa; Imani wanayoimwilisha katika maisha adili na maisha ya sala. Imani inapaswa kuoneshwa katika matendo na kuacha mtindo wa maisha ya undumilakuwili kwa kuendelea kuambata imani za kishirikina. Umefika wakati pia wa kupambana na rushwa ambayo imekuwa ni saratani kwa wananchi wengi wa Uganda ili kweli jamii iweze kusimikwa katika misingi ya haki na amani.

Askofu Giuseppe  Franzelli wa Jimbo Katoliki la Lira, Uganda anakaza kusema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uganda itasaidia kuleta mwanga wa matumaini katika maisha na utume wa Familia ya Mungu nchini Uganda. Asaidie kukuza mema na matakatifu, awaombee Waganda ujasiri wa kuachana na mambo yote yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Uganda: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.