2015-11-24 15:29:00

Dini ina dhamana nyeti katika ustawi na maendeleo ya binadamu!


Kardinali Antonio Maria Veglio’, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum anasikitika kusema kwamba, wakati huu kuna mwelekeo kwa baadhi ya watu kudhani kwamba, dini imekuwa na mwelekeo hasi katika maisha ya watu kwani vitendo vingi vya kigaidi vinafanywa kwa kutumia mwamvuli wa dini. Lakini, kimsingi dini zinapaswa kuwa ni chombo makini cha kusaidia kuhamasisha mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu na kamwe kisiwe ni sababu ya watu kugawanyika na kupigana!

Kardinali Veglio’ ameyasema haya hivi karibuni wakati wa kuhitimisha mkutano wa wadau mbali mbali uliokuwa unajadili kuhusu dhana ya uhamiaji wa watu unaofumbatwa katika dini na tamaduni mbali mbali, huko Pozzalo, Ragusa. Dini ina mchango mkubwa katika kuwahamasisha watu kujenga umoja na mshikamano wa dhati kwa kupokeana jinsi walivyo na kwamba, tofauti zao ni utajiri mkubwa katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya wengi.

Watu wanapaswa kuwaona wakimbizi na wahamiaji kuwa ni rasilimali na nguvu kazi inayochangia katika ustawi na maendeleo ya watu na kwamba, watu hawa si mzigo, bali wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Umoja na mshikamano unajikita katika mantiki kwamba, wote ni watoto wa Mungu wanaounda familia ya binadamu. Serikali ziwasaidie wakimbizi na wahamiaji kuwajibika barabara kwa kujikita katika sheria, kanuni na taratibu za nchi husika, bila kusahau kuwapatia haki zao msingi.

Kardinali Veglio’ anakaza kusema, Kwa Kanisa, wahamiaji na wakimbizi ni chachu ya ujenzi wa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume! Ndani ya Kanisa hakuna mgeni wala mkimbizi, kila mtu anapaswa kuheshimiwa ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa Watoto wa Mungu. Mashambulizi na vitendo vya kigaidi vinavyojitokeza sehemu mbali mbali za dunia, vinawajengea watu hofu na kishawishi cha kutaka kujifungia ndani mwao na hivyo kukosa ile fadhila ya ukarimu kwa wageni na wahijati wanaotaka kusalimisha maisha yao. Watu wanaoishi katika nchi zilizoendelea watambue kwamba, wanayo dhamana kubwa ya kutumia utajiri na rasilimali yao kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.