2015-11-18 08:21:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu


Tunakuleteeni habari njema ya furaha tunapotafakari pamoja ujumbe wa Neno aliyefanyika mwili, Mfalme wa mbingu na nchi. Ni Dominika ya 34 ya mwaka B iliyo pia Sherehe ya Yesu Krist mfalme wa ulimwengu. Kanisa linashangilia na kusherehekea utukufu wa Mwana wa Mungu, Yesu Kristo mfalme. Kanisa linatangaza daima utawala na enzi ni vya Yesu Kristo mfalme na hivi lajiweka chini ya uongozi wake aliye kichwa na mwanga katika safari ya kuelekea mbinguni. Pamoja na tangazo hilo Kanisa latuhimiza kumfuata Yesu Kristo mfalme, kukiri ukuu wake wazi wazi machoni pa mataifa lililo hasa lengo la sherehe hii.

Katika Injili ya Mtakatifu Yohane tunakutana na Pilato anayeweka swali mbele ya Kristo akisema “Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Na Bwana kwa unyenyekevu mkuu, anajibu akisema wewe wasema hivi kwa nafsi yako au watu wengine wamekuambia hivi!! Jibu la namna hii lilikwishatolewa pia kwa Kayafa katika Injili ya Marko. Wanamaandiko matakatifu, wanasema Bwana, katika Injili ya Marko atashindilia kwa mkazo jibu lake akinukuu maneno toka Nabii Danieli yanayolenga nafsi yake yeye mwenyewe, akisema “mtamwona Mwana wa mtu ameketi kuume kwa mwenye nguvu akishuka katika mawingu toka mbinguni”. Ni kutokana na mkazo huo Mama Kanisa amechagua somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Nabii Danieli, ili lituongoze katika kutafakari ufalme wa Kristu ulio kabla ya Agano la Kale na unasafiri na kuongoza Agano hilo na kulisalimisha katika Agano Jipya na kisha milele mbinguni.

Kwa hakika Somo la kwanza linatanguliwa na mazingira ya falme za kidunia zinazowakilishwa na wanyama wakubwa wanne ambao wanaibuka toka baharini kila mmoja baada ya mwingine, wakisimama kwa miguu miwili na kisha kupewa akili ya binadamu. Wanyama hawa kwa hakika ni hatari kwa maisha na kwa jinsi hiyo basi leo wanawakilisha falme fidhuli zinazodhulumu haki za wananchi kama tushuhudiavyo. Ni katika mazingira hayo ghafla tunaona mabadiliko ambayo yanajitokeza katika somo la kwanza. Ndiyo kusema, anaonekana mmoja aliye mfano wa mwanadamu akija katika mawingu na kumkaribia mzee wa siku na kukabidhiwa mamlaka na utukufu na kila aina ya uzuri wa milele. 

Jambo hili mara moja inatupeleka kuona matunda baada ya mateso ya mwanadamu hapa duniani, anavyofurahia utukufu mbinguni. Kwa hakika wanamaandiko wanasema mtu huyu anayekabidhiwa utukufu katika Agano la Kale ni taifa la Israeli na katika Agano Jipya ni Yesu Kristo Mfalme, kiongozi wa historia nzima ya mwanadamu na ulimwengu wote.

Mpendwa mwanatafakari, sote twatambua kuwa, Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme mbele ya watesi wake anajipambanua kama Mwana wa Mtu, alama na ashilio la umwilisho, Kristo anaingia katika historia ya mwanadamu lakini pia anakuwa juu ya historia na kuiongoza mpaka ukamilifu wake. Kwa hakika uaguzi wa Nabii Danieli unakamilika katika Bwana wa Agano Jipya. Ndiyo kusema, Kristo si wa Agano Jipya tu bali anakatiza historia nzima ya ulimwengu toka mwanzo wake hadi mwisho wake (Kristo mwaguliwa na Kristo aliyemwilishwa).

Kristo anayetawala historia ni yuleyule ambaye ni mnyenyekevu na mteswa kama tunavyopata kutafakari katika somo la II likisema yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika Damu yake na kutufanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu. Sifa hii ambayo anapewa Bwana katika Kitabu cha Ufunuo inajitokeza katika Injili pale ambapo Bwana ni Mchungaji mwema, Bwana ni mpole na mnyenykevu wa moyo, Bwana anapowaambia wanafunzi wake kwamba siwaiti tena watumishi bali rafiki zangu. Ndiyo kusema Kristo ni mfalme wa amani, ni mkombozi, ni rafiki yetu kwa maana ya kutusindikiza katika kukabiliana na historia yetu hadi tutakapofika mbinguni.

Mpendwa mwana wa Mungu, Mama Kanisa anatualika katika Sherehe hii ya Yesu Kristo mfalme, kwanza kumtambua Bwana kuwa kiongozi wa historia na maisha yetu kwa ujumla, lakini hasa kumfahamu ktk ukamilifu wake, yaani mtu kweli na Mungu kweli. Tabia yake hiyo ni lazima kuitunza katika vizazi vyote mpaka yatakapotimia. Kristo yu katikati yetu kama rafiki na Mfalme, Bwana na Mkombozi. Wito kwetu ni kumpokea kwa kuyaishi mapenzi yake tukijaribu kutumikia ili kuleta ustawi katika maisha ya watu.

Mpendwa mwanatafakari, ufalme wa Kristo tutauishi kwa kushuhudia kwa dhati imani Katoliki, imani tendaji, imani inayokuza ubatizo hadi mwisho wa nyakati. Ni kubaki katika pendo la Mwana wa Mungu katika kuhudumu walio wake, walio wahitaji na kuishi huruma yake isiyo na mwisho. Tunaposherehekea Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wetu tukumbuke kuwa yeye anapaswa kutawala katika familia zetu zote, katika maneno yetu na matendo yetu. Maneno kama “mteja ni mfalme” yafaa kuangaliwa vizuri kama kweli yanakuza ufalme wa Kristo au ufalme wetu sisi wenyewe na ufalme wa jumuiya fidhuli na nyonyaji katika ulimwengu huu.

Nikutakieni heri na baraka katika Sherehe hii ambayo lengo lake ni kukuza Ufalme wa Kristu maishani mwetu tukiongozwa naye aliye mfalme wa amani. Tumsifu Yesu Kristo Mfalme. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S. 








All the contents on this site are copyrighted ©.