2015-11-18 12:08:00

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika inaendelea kama ilivyopangwa!


Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Gazeti la Avvenire linalomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, Jumuiya ya Kimataifa pamoja na wapenda amani wote wameshtushwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyojitokeza nchini Ufaransa na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hakuna mtu au taifa ambalo linaweza kujihakikishia usalama wake kwa asilimia mia moja, jambo la msingi ni watu kuwa waangalifu zaidi na kamwe wasimezwe na woga na hofu zisizo na mvuto wala mashiko!

Ziara ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 25- 30 Novemba 2015 kwa kutembelea Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati inatarajiwa kutekelezwa kama ilivyopangwa na kwamba, kwa sasa hakuna mabadiliko yoyote. Kuna changamoto ya ulinzi na usalama Afrika ya Kati, lakini Baba Mtakatifu ameipatia kipaumbele cha kwanza kwani anataka kuwaimarisha ndugu zake katika imani, mapendo na matumaini, tayari kujikita katika majadiliano na ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana.

Kuhusu hali ya ulinzi na usalama mjini Vatican anasema, wasi wasi na hofu ipo, lakini mambo haya yanapaswa kukabiliwa kwa ujasiri pasi na kukata wala kukatishwa tamaa, jambo ambalo linaendelea kuoneshwa na Ufaransa pamoja na mataifa mengine. Lengo la magaidi ni kupandikiza mbegu ya hofu na wasi wasi miongoni mwa watu. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwa na ujasiri na mbinu mpya za kupambana na vitendo vya kigaidi.

Kardinali Pietro Parolin anasema, safari ya kikazi iliyokuwa imepangwa na Rais Hassan Rohan wa Iran ili kutembelea Vatican ilifutwa kutokana na sababu za ulinzi na usalama na kwamba, malango ya Vatican yako wazi, anaweza kuja Vatican wakati atakapoona kwamba, inafaa zaidi. Vatican inapenda kuonesha mshikamano na majadiliano na nchi ya Iran kwa ajili ya mafao ya wengi.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Kardinali Parolin inaweza kupambana na vitendo vya kigaidi kwa kushirikiana kwa dhati na kwamba, kila serikali inawajibu wa kulinda amani na usalama wa raia wake sanjari na kuhakikisha kwamba, inatumia njia muafaka ili kutekeleza lengo hili msingi na muhimu katika mchakato wa maendeleo na ustawi wa jamii. Kuna haja ya kuendeleza mchakato wa majadiliano kati ya watu, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano; mambo ambayo yanaweza kuchukua muda mrefu kutekelezwa, lakini hatima yake ni amani, utulivu na upatanisho.

Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kufikia maamuzi msingi katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi, kwa kuzingatia sheria za kimataifa, haki msingi za binadamu kwa kuendelea kushirikiana pamoja na kudumisha majadiliano kati ya watu, ili kweli maamuzi yanayofikiwa yaweze kutekelezwa na watu wengi zaidi. Viongozi wa kidini wanayo dhamana mahususi katika kusaidia majiundo ya dhamiri za watu ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia haki, amani na maridhiano ya kweli.

Kardinali Parolin anakaza kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko yatazinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2015 yataendelea kama yalivyopangwa na wala hakuna sababu ya msingi ya kutaka kufuta wala kuhailishwa kwa maadhimisho haya. Hiki ni kipindi cha kuendelea kuhimiza umuhimu wa majadiliano, haki, amani na upatanisho. Maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kujikita katika majadiliano ya kidini kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji juu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, “Misericordiae vultus” Uso wa huruma.

Mwaka Mtakatifu iwe ni fursa muhimu ya kuwaunganisha waamini wa dini mbali mbali ili kwa pamoja waweze kuondokana na nyanyaso, ubaguzi na vurugu zinazosababishwa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini. Dini zote hizi zinaonesha utajiri mkubwa katika dhana ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei yahuruma ya Mungu waamini wa dini hizi wanaweza kukutana kama sehemu ya majadiliano ya kidini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.