2015-11-17 08:19:00

Vatican na Zambia waadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 12 Novemba 2015 amekuwa na ziara ya kikazi nchini Zambia kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Uhuru wa Zambia sanjari na Miaka 50 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Zambia. Mahusiano haya yalianzishwa na Mwenyeheri Paulo VI kunako tarehe 27 Oktoba 1965 katika Waraka wake wa kitume “Africae gentes”.

Akiwa nchini Zambia, Askofu mkuu Gallagher amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa, Serikali ya Zambia chini ya uongozi wa Rais Edgar Chagwa Lungu pamoja na Mabalozi na wawakilishi wa Jumuiya ya Kimataifa nchini Zambia. Askofu mkuu Gallagher amebahatika kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Makanisa kadhaa kwa kukazia umuhimu wa Zambia kuendelea kuwa ni udongo mzuri kwa ajili ya kupandikiza Habari Njema ya Wokovu. Akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Majandokasisi wa Seminari kuu ya Mtakatifu Dominiko, Askofu mkuu Gallagher amewataka Waseminari hao kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha na wito wao, daima wakilenga juu zaidi kwa kuonesha upendo na uaminifu.

Akizungumza na Rais Edgar Chagwa Lungu, wakati wa kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Zambia na Vatican, Askofu mkuu Galagher amepongeza mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya Vatican na Zambia pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Zambia. Kanisa kwa namna ya pekee, limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni  mwa jamii. Mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili yanalenga kwa namna ya pekee kudumisha na kuimarisha huduma kwa familia ya binadamu, kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu, haki na amani. Serikali ya Zambia kwa namna ya pekee, inalipongeza Kanisa Katoliki kwa  mchango wake katika maendeleo ya wananchi wengi wa Zambia, lakini zaidi katika sekta ya elimu na afya.

Askofu mkuu Gallagher, amepata pia nafasi ya kutembelea nchini Malawi, huku akiongozana na Askofu mkuu Julio Murat, Balozi wa Vatican nchini Zambia na Malawi, ambako amepokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Malawi. Viongozi hawa katika mazungumzo yao wamegusia kwa namna ya pekee, mambo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu ya wananchi wa Malawi, ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kwa namna ya pekee baa la njaa na umaskini.

Askofu mkuu Tarcisius Zizaye, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, amemshukuru kwa namna ya pekee kabisa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuijali Familia ya Mungu nchini Malawi katika shida na mahangaiko yake; wakati wa raha na machungu. Kwa upande wake, Askofu mkuu Richard Paul Gallagher amewasilisha salam za Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuonesha moyo wake wa upendo na sala kwa wale wote walioathirika kutokana na mafuriko pamoja na ukame wa kutisha nchini Malawi. Askofu mkuu Gallagher katika Ibada ya Misa Takatifu, akiwa Malawi, amewataka waamini kuwa ni mashuhuda wa mwanga wa Injili ya Kristo, kwa kuonesha mshikamano na huduma kwa maskini na wagonjwa, hasa wale wanaoteseka kutokana na ukimwi. Maaskofu wa Malawi wamemshirikisha Askofu mkuu Gallagher maisha na utume wa Kanisa nchini Malawi pamoja na changamoto wanazoendelea kukabiliana nazo.

Askofu mkuu Gallagher akiwa nchini Malawi amekutana na kuzungumza na Rais Peter Mutharika wa Malawi aliyekuwa ameambatana na viongozi wa Serikali pamoja na Kanisa. Kwa muda wa miaka arobaini na tisa, Malawi imekuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Katika kipindi cha miaka yote hii, Kanisa limekuwa mdau wa pekee kabisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Malawi: kiroho na kimwili. Kanisa limesaidia kudumisha mchakato wa utawala bora na demokrasia nchini Malawi.

Rais Mutharika amelishukuru kwa namna ya pekee kabisa Kanisa Katoliki kwa msaada mkubwa lililotoa kwa wananchi wa Malawi walipokumbwa na mafuriko pamoja na ukame wa kutisha. Askofu mkuu Gallagher ametumia nafasi hii kuwasilisha pia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa wananchi wa Malawi. Kabla ya kuondoka kutoka Malawi, Askofu mkuu Gallagher alipata nafasi ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Watawa wa ndani wa Mtakatifu Clara kwa kuwataka kuwa kweli ni mashuhuda amini wa maisha ya kuwekwa wakfu, kwa kufuata mfano wa karama na moyo wa Mtakatifu Clara wa Assisi. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher tayari amerejea mjini Vatican na anaendelea “kudunda mzigo kama kawa”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.