2015-11-16 08:05:00

Wananchi wa Kenya wanahamasishwa kujitokeza kwa wingi kumpokea Papa Francisko


Askofu Alfred Rotich, Mwenyekiti wa Tume ya Mapokezi ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Kenya kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa kuchangia kwa hali na mali katika mapokezo ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya. Sehemu kubwa ya maandalizi tayari imekamilika na kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwa kushirikiana na Serikali wanaendelea kukamilisha mambo mengine yaliyobaki!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaipongeza Familia ya Mungu nchini Kenya kwa kuendelea kuchangia kwa hali na mali ili kufanikisha mapokezi ya Baba Mtakatifu Francisko anapotembelea Kenya ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, tayari kwa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana ili kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Kenya sanjari na kuimarisha haki, amani na maridhiano.

Inakadiriwa kwamba, watu zaidi ya million 1. 4 kutoka sehemu mbali mbali za Kenya wanatarajiwa kuhudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya, kabla ya kuondoka kuelekea Uganda. Kuna vituo 20, 000 vya sala ambavyo vimetayarishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ili kuwawezesha waamini kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya sala wakati wa hija yake ya kichungaji Barani Afrika.

Askofu Alfred Rotich anasema hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya ni Baraka hata kwa Familia ya Mungu kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, yaani AMECEA, kwani kutakuwepo na Makardinali na Maaskofu 60; Wakleri wanakadiriwa kuwa ni 9, 000. Kuna Shirikisho la kwaya 12 litakaloshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko itarushwa moja kwa moja kwenye vituo mbali mbali vya Televisheni, Radio na Mitandao ya kijamii ili kuwawezesha watu kujionea wenyewe kile kinachoendelea wakati wa hija hii ya kitume, inayopania  kuimarisha Familia ya Mungu nchini Kenya katika imani, matumaini na mapendo! Askofu Rotich anawahimiza wananchi wote wa Kenya kushikamana katika misingi ya haki, amani na maridhiano, ili kufanikisha hija ya Baba Mtakatifu Francisko.Hija ya Baba Mtakatifu nchini Kenya uwe ni msingi thabiti wa amani na utulivu. Wananchi wote wa Kenya watambue kwamba, ni watoto wa Mungu na tofauti zao za kikabila, kidini au mahali anapotoka mtu isiwe ni sababu na chanzo cha kuvunjika kwa amani na utulivu.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta inawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi kumpokea na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Francisko atakapowasili nchini Kenya kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 Novemba 2015. Baba Mtakatifu anataka kukutana, kuzungumza na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na Familia ya Mungu nchini Kenya. Wananchi wajitokeze barabarani katika maeneo atakakokuwa anapitia Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume nchini Kenya, tukio ambalo linapaswa kuwa kweli ni kumbu kumbu endelevu miongoni mwa wananchi wa Kenya.

Serikali inapenda kuwahakikishia ulinzi na usalama wananchi wote wa Kenya. Baba Mtakatifu ni kiongozi mnyenyekevu anayependa kuwa kati ya watu kwa ajili ya kuwahudumia watu, ili waweze kushikamana na kupendana kama ndugu wamoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA.








All the contents on this site are copyrighted ©.