2015-11-16 15:02:00

Kanisa linachangamotishwa kuwa fukara ili kuwahudumia vyema maskini!


Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili walipotia sahihi katika mktaba wa Macatacombs, ili Kanisa liweze kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini katika maisha na utume wake. Padre Felix Mushobozi, C.PP.S kutoka Tume ya haki na amani ya Shirikisho la Wakuu wa Mashirika anafafanua maana ya mktaba huu, lengo, umuhimu na changamoto zake kwa Kanisa Barani Afrika.

Katika Makala haya Padre Mushobozi anaelezea kwa ufupi historia na lengo la kuanzishwa kwa Macatacomb pamoja na changamoto iliyotolewa na Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1965 alipokazia umuhimu wa Macatacomb katika maisha na utume wa Kanisa alikaza kusema, hapa Kanisa lilivuliwa nguvu za kibinadamu, Kanisa likawa maskini na nyenyekevu; Kanisa likamwambata na kumcha Mungu; hapa Kanisa lilidhulumiwa na kuibuka kuwa shujaa!

Katika Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipoweka sahihi Mktaba wa Macatacomb, watawa wa Mashirika mbali mbali wameshiriki kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Njia ya Msalaba. Kumekuwepo na semina pamoja makongamano mbali mbali, ili kufafanua umuhimu wa Kanisa kuwa fukara kwa ajili ya kuwahudumia maskini wa hali na kipato. Mkataba huu ni changamoto kubwa kwa Kanisa Barani Afrika ambalo kwa kiasi kikubwa linawahudumia maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linakuwa kati ya watu kwa ajili ya huduma makini kwa watu, ili hatimaye waweze kufika mbinguni kwenye maisha ya uzima wa milele. Ni dhamana kubwa ya Kanisa Barani Afrika kushughulikia haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu.

Na Padre Felix Mushobozi, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.