2015-11-14 14:58:00

Mashambulizi ya kigaidi yatikisa Jiji la Paris, Ufaransa


Baba Mtakatifu Francisko ameonesha masikitiko makuu kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyojitokeza Paris, Ufaransa, Ijumaa usiku tarehe 13 Novemba 2015 na kusababisha zaidi ya watu 128 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 250 kupata majeraha makubwa, tukio ambalo limewashtua watu wengi ndani na nje ya nchi ya Ufaransa. Baba Mtakatifu ameyasema haya wakati alipokuwa anazungumza na wajumbe wa Shirika la Wayesuit linalotoa huduma kwa wakimbizi sehemu mbali mbali za dunia, wakati huu wanapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 35 tangu lilipoanzishwa na Padre Pedro Arrupe, Mkuu wa Shirika la Wayesuit kwa wakati ule!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutuma salam zake za rambi rambi kwa Rais wa Ufaransa pamoja na wananchi wote wa Ufaransa kwa kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa familia zilizoguswa na mashambulizi haya ya kigaidi, yaliyopelekea watu kupoteza maisha na wengine kupata majeraha makubwa. Ni mashambulizi dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kamwe matumizi ya nguvu hayataweza kusaidia kutatua matatizo na changamoto zinazomkabili binadamu!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali kuwaombea wote waliofariki dunia katika mashambulizi haya waweze kuonja huruma ya Mwenyezi Mungu na wale waliopata majeraha waweze kupona haraka na hatimaye, kuendelea na shughuli zao za kawaida. Anawatia shime wale wote wanaoendelea kutoa msaada kwa waathirika, ili watekeleze dhamana hii nyeti kwa ujasiri na imani thabiti.

Naye Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambi rambi Kardinali  Andrè Ving-Trois, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa kutokana na mashambulizi ya kigaidi. Anapenda kuwahakikishia wote walioguswa na matukio haya uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya sala na sadaka yake.

Kwa upande wake, Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Vatican inaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi matukio haya ya kigaidi na chuki kati ya watu na kwamba, Vatican inalaani kwa nguvu zote vitendo vinavyodhalilisha na kunyanyasa utu wa binadamu. Shutuma kama hizi zinatolewa pia na watu wote wenye mapenzi mema na wanaotaka amani na utulivu kutawala miongoni mwa jamii ya watu. Kwa vile mashambulizi haya yanaelekezwa dhidi ya amani, kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuungana kwa pamoja kulaani vitendo hivi vinavyokumbatia utamaduni wa kifo!

Naye Rais Barack Obama wa Marekani anakaza kusema Serikali yake itaendelea kuwatafuta na kuwaadhibu watu wanaojihusisha na vitendo vya kigaidi kwa kuhakikisha kwamba, wanafikishwa kwenye mkondo wa sheria. Anaapa kwamba, ataendelea kula sahani moja na magaidi hadi kieleweke!

Kwa namna ya pekee Kardinali Andrè Vingt-Trois, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Paris anasikitika kusema, baada ya mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kusikika sehemu mbali mbali za dunia katika kipindi cha siku za hivi karibuni, Ufaransa nayo imetikiswa kwa kushambuliwa tena na magaidi wenye misimamo mikali ya kiimani. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali ili kuwaombea wote waliofariki dunia katika mashambulizi haya ya kinyama na majeruhi waweze kupona na kurejea tena katika shughuli zao. Kardinali Vingt-Trois anawataka viongozi wa Kanisa kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya Kanisa na nyumba za Ibada.

Jumapili itakuwa ni siku ya maombolezo na jioni, ataadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wote walipoteza maisha yao kutokana na mashambulizi haya ya kigaidi. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuachana na tabia ya chuki na hali ya kutaka kulipiza kisasi na badala yake, waombe neema ya kuwa ni vyombo na wajenzi wa haki, amani na upatanisho. Kamwe waamini wasipoteze matumaini katika amani kwa kujenga na kujikita katika misingi ya haki!

Wakati huo huo, Kardinali Oswald Gracias, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mumbai, India, wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu kitaifa nchini India, amewaalika wajumbe wa kongamano hili kukaa kimya kwa kitambo ili kusali na kuwaombea wote waliopoteza maisha kutokana na mashambulizi ya kigaidi. Wamewakumbuka wanafamilia wao, ili waweze kuwa imara katika kipindi hiki cha majonzi makuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.