2015-11-13 14:52:00

Ninyi mliobahatika kuwa na utajiri waonjesheni wakimbizi na wahamiaji upendo!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 13 Novemba 2015 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Romano Guardini wanaohudhuria mkutano wa kumbu kumbu ya miaka 130 tangu alipozaliwa; mkutano ambao umeandaliwa na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko hapa mjini Roma. Romano Guardini ni kati ya wasomi wa hali ya juu kwa nyakati hizi na kwamba, Mfuko wake unapania kuendeleza mawazo na fikira zake katika mchakato wa majadiliano: kisiasa, kitamaduni na sayansi ya maisha ya kila siku. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, harakati hizi zitasaidia kuzaa matunda kwa wakati wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Romano Guardini, Padre alikuwa ni msomi aliyeweza kusikiliza kilio cha watu, akawasaidia kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Kwa mtu anayetubu, hana sababu ya kuogopa kwani Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, yuko tayari kusamahe na kusahau.

Toba inaimarisha imani na utashi wa mtu na kwamba, hata dunia yote ikitubu na kumwongokea Mungu, yuko tayari kusamahe. Hakuna dhambi inayoweza kutendwa na mwanadamu ambayo kamwe haiwezi kusamehewa na Mungu. Katika maungano na toba ya ndani, mwamini anaonja mabadiliko na kupata matumaini mapya. Hekima na upendo wa Mungu vinajionesha kwa namna ya pekee kwa mwamini anayeambata imani yake kwa dhati pamoja na kujiaminisha kwa Mungu kwani maisha yake daima yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii waamini wanaweza kuonja wema wa Mungu aliye hai katika umoja wao.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwambakwa Guardini “umoja ulio hai” na Mwenyezi Mungu unajidhihirisha katika mahusiano ya watu pamoja na dunia inayowazunguka. Huu ni umoja unaosimikwa katika maisha ya viumbe hai na kwa namna ya pekee kabisa binadamu aliye hai na wala si watu wa kufikirika. Maisha ya binadamu yanafungamana na mazingira halisi na kwamba, mwanadamu ni muhtasari wa mambo msingi na kwamba, wao ni kielelezo cha kazi ya Mwenyezi Mungu inayogusa Fumbo la maisha yake.

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa mkutano huu kutafakari matukio mbali mbali katika maisha, ili kugundua mkono wa Mungu unaotenda kazi duniani. Watu wanaweza kumfahamu Mungu na Hekima yake aliyotuma Ulaya, Bara lenye utajiri ili kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu; kuwatunza wageni na kuwavisha walio uchi.

Jambo hili linawezekana ikiwa kama watu wote watajisikia kuwa ni wamoja na kwa njia ya hii wanaweza kuonesha ukarimu, lakini ikiwa kama wamegawanyika na kusambaratika, kila kundi litajitahidi kutafuta mafao yake na hapa hapakuwepo tena na mwendelezo. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hotuba yake kwa kuwashukuru wajumbe wote kwa uwepo wao na kwa njia ya kazi ya Guardini wanaweza kupata nafasi ya kufahamu kwa undani zaidi tunu msingi za maisha ya Kikristo, kitamaduni na kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.