2015-11-07 10:50:00

Changamoto katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Jubilei ya huruma ya Mungu


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu ni muda muafaka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema Jimbo kuu la Roma, kusimama, kutafakari na kupiga magoti, ili kila mmoja aweze kutoa mchango wake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jiji la Roma: kiroho na kimwili. Ni changamoto ya kutekeleza wito na wajibu wa kila mtu, ili kujibu kiu ya matumaini ya wananchi wa Roma. Hii ni changamoto inayotolewa na Kardinali Agostino Vallini katika barua yake ya kichungaji kwa Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu; Mwaka uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko. Jiji la Roma linakabiliwa na changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa shughuli zake na huduma kwa jamii.

Kuna saratani ya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma; umaskini na hali ya watu kukata na kujikatia tamaa; athari za myumbo wa uchumi kimataifa na kitaifa; ukosefu wa mikakati na sera makini ya ulinzi na usalama; kuongezeka kwa umaskini na ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana pamoja na kinzani za kijamii.  Kuna ongezeko la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao, lakini wanakumbana na kinzani na baadhi ya watu kutotaka kuwaonjesha huruma na upendo. Zote hizi ni changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu, ili kuonesha dalili za uwepo na ukaribu wa Mungu kwa wote wanaoteseka. Ni mwaliko wa kujikita katika mambo msingi zaidi katika maisha ya mwanadamu pasi na kupoteza upeo, ili watu wengi zaidi waweze kuonja huruma ya Mungu ambayo ni utimilifu wa haki katika ulimwengu geugeu!

Kardinali Vallini anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni mashuhuda wa mng’ao wa mwanga angafu wa maisha na furaha ya watoto wa Mungu, kwa kutambua kwamba, Kanisa la Roma ni msingi wa upendo kwa Makanisa mengine yote. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa Katoliki limewekeza rasilimali kubwa ya watu na vitu Jijini Roma, inayopaswa kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma, iwe ni kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya watu wa rika mbali mbali, kwa kusaidiana na kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu. Watu washikamane na kusaidiana; wazee kwa vijana wa kizazi kipya.

Kardinali Vallini anasema, kwa sasa Jiji la Roma linakabiliwa na changamoto kadhaa zinazopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Kwanza kabisa ni umaskini wa hali na kipato unaoendelea kuwanyanyasa wananchi wengi, kiasi hata cha baadhi ya familia kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Haya ni matokeo ya ukosefu wa fursa za ajira na sera makini katika ustawi na maendeleo ya watu. Kuna idadi kubwa ya watu wasiokuwa na makazi bora.

Pili, kuna ongezeko kubwa la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, hapa waamini wanahamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu dhidi ya nyanyaso na dhuluma zinazofanywa kwa misingi ya udini, utaifa na ukabila; kwani yote haya ni matokeo ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Tatu, kuna haja ya kujikita katika sera na mikakati bora ya elimu kwa kutambua kwamba, Jamii inapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara katika masuala ya elimu na malezi kwa vijana wa kizazi kipya: kiutu, kimaadili na kitamaduni badala ya kutafuta faida kubwa inayojificha katika uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka.

Jambo la nne anasema Kardinali Vallini, ni umuhimu wa kuwa na matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Mara nyingi, vyombo vya habari vimekuwa vikipotosha umma kwa kuonesha picha ya maisha ambayo hailandani kabisa na uhalisia wa maisha ya wananchi wengi wa Italia. Kanisa linapenda kutoa mchango wake katika kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa kujikita katika kanuni maadili, weledi na uwajibikaji.

Kardinali Agostino Vallini, anahitimisha barua yake ya kichungaji kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma kwa kusema kwamba, kuna haja ya kuanza kuwafunda viongozi wa kisiasa na kijamii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na Jamii kwa siku za usoni. Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa umakini zaidi kwa njia ya vyama vya kitume vinavyosimamiwa na kuongozwa na waamini walei. Hii ni changamoto ya kujenga utamaduni wa majadiliano katika kukuza na kudumisha Mafundisho Jamii ya Kanisa hata na wale ambao si waamini wa Kanisa Katoliki, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Hivi ndivyo Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma inavyoweza kuadhimisha vyema Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, kwa kuambata na kuwamegea wengine huruma hii ambayo kimsingi ni kielelezo cha upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.