2015-11-05 15:12:00

Jamani uchaguzi umekwisha, Rais ni Dr. John Pombe Magufuli, Kazi kama kawa!


Watanzania Alhamisi tarehe 5 Novemba 2015 wameshuhudia Dr. John Pombe Joseph Magufuli akiapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mama Samia Suluhu Hassan akiapishwa kuwa ni Makamu wa Rais, katika tukio ambalo limeshuhudiwa na umati mkubwa wa watu na wengine kufuatilia tukio hili katika vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Rais Magufuli baada ya kuapishwa, akaombewa sala na dua na viongozi mbali mbali wa dini nchini Tanzania, kati yao ni Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Viongozi wa dini katika sala na dua zao, wamemshukuru Mungu kwa kuwajalia watanzania paji la amani na utulivu; wamemwomba msamaha kwa mapungufu ya kibinadamu yaliyojitokeza wakati wa kampeni. Wamewaombea viongozi wapya wawe na busara, hekima na ujasiri wa kuwatetea na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watanzania walio wengi. Viongozi wa kidini wamewashukuru viongozi wa awamu ya tano na kwamba, sasa watanzania wanapaswa kujikita katika upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja na kwamba, uchaguzi umekwisha, sasa ni kazi tu!

Rais Magufuli amepigiwa mizinga ishirini na moja na baadaye kukagua gwaride, kama Amiri Jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama. Kisha vikosi hivi vikapita mbele ya umati wa watanzania kwa ukakamavu mkubwa! Watanzania wengi wamesikika wakisema, kweli hapa kazi tu! Katika hotuba yake ya shukrani, Rais Magufuli amewashukuru viongozi mbali mbali waliowahi kuiongoza Tanzania hadi kufikia wakati huu. Amemshukuru Mungu kwa kuiwezesha Tanzania kufanya uchaguzi kwa amani na watanzania kushudhia viongozi wakikabidhiana madaraka kwa amani na utulivu.

Rais Magufuli amewataka wananchi wa Zanzibar kuwa na moyo wa subira wakati huu wanapopita katika kipindi kigumu cha historia ya nchi yao, kilichojaa majaribu makubwa na kwamba, anamwomba Mwenyezi Mungu ili waweze kuvuka salama na kwa amani. Anasema wameipokea dhamana ya kuiongoza Tanzania kwa unyenyekevu mkubwa na wanamwomba Mungu awajalie moyo na hekima ya kuweza kutekeleza dhamana hii kwa: akili, juhudi na maarifa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Wanatambua changamoto kubwa zilizoko mbele yao, lakini wanapenda kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika utekelezaji wa dhamana hii.

Rais Magufuli anawashukuru na kuwapongeza viongozi wa vyama vya upinzani waliompatia changamoto nyingi na kwamba, kuna mengi ameweza kujifunza kutoka kwao na watambue kwamba, wao si wapinzani bali walikuwa ni washindani, Tanzania ndiyo iliyoshinda. Wanapaswa kuunganisha nguvu zao ili kuwatumikia watanzania bila kujali udini, ukabila au mahali anapotoka mtu. Huu ni wakati wa kushikamana ili kujenga umoja na amani.

Dr. John Pombe Magufuli amewashukuru wadau mbali mbali kwa kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Tanzania na kuwaomba wabunge kushirikiana kwa pamoja ili kutekeleza mikakati ya maendeleo kwa watanzania wote. Kwa namna ya pekee kabisa amempongeza Rais mstaafu Benjamini William Mkapa aliyemwona akiwa kijana wa umri wa miaka 35 akamkabidhi dhamana ya kuwa Naibu Waziri, leo hii ni mtu mzima umri wa miaka 56, amepewa dhamana ya kuiongoza Tanzania kama Rais.

Hii ni heshima kubwa na kwamba, atajitahidi kuendeleza mema na mazuri kutoka kwa viongozi waliomtangulia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania. Uchaguzi umekwisha, sasa kazi kwenda mbele! Sherehe hizi zimehudhuriwa na viongozi kutoka nchi mbali mbali za Afrika, lakini kwa namna ya pekee alikuwepo Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Mvua kubwa imenyeesha Dar es Salaam, kielelezo cha baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini wananchi wamevumilia hadi tukio zima kukamilika! Kumekuwepo na umati mkubwa wa wawakilishi kutoka katika nchi marafiki!

Imeandaliwa na Padre Agapito Mhando na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.