2015-11-04 09:01:00

Kanisa mahalia lioneshe ushirikiano wa dhati na Wamissionari!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa uwepo na ushuhuda wa Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu katika kipindi cha miaka 200 tangu Shirika lao lilipoanzishwa. Anawapongeza Wamissionari wa C.PP.S nchini Tanzania kwa mchango wao katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. C.PP.S. imechangia sana katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Kanda ya Kati nchini Tanzania katika sekta ya elimu, maji, afya na maendeleo endelevu, hususan katika mikoa ya Singida na Dodoma.

Askofu mkuu Ruwa’ichi ambaye amewahi kulihudumia Jimbo Katoliki la Dodoma anakaza kusema, Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu walifika nchini Tanzania kwa mwaliko wa Marehemu Askofu Jeremiah Pesche, Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Dodoma. Wakapata ushirikiano wa dhati kutoka kwa Kanisa mahalia na hivyo kufanikiwa kuendeleza utume wao Wilayani Manyoni, Jimbo Katoliki Singida. Leo hii Manyoni ina sura mpya, ikilinganishwa na miaka hamsini iliyopita.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anawapongeza Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika lao, kielelezo makini cha neema, baraka na ukomavu. Ni matumaini yake kwa wataendelea kuimarisha ukomavu na kuushuhudia katika maisha na utume wao. Anawapongeza kwa kuzindua Kanda mpya ya C.PP.S. nchini Tanzania, kielelezo pia cha ukomavu na uwepo wa miito ya kitawa na kimissionari, tayari kuendeleza maisha na utume wa Shirika ndani na nje ya Tanzania. Miito hii ni chachu ya nguvu na matumaini kwa leo na kesho.

Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Ruwa’ichi anawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati, ili Wamissionari hawa waweze kutekeleza dhamana na utume wao wa Uinjilishaji kwa kuguswa na kilio cha damu! Anampongeza Mheshimiwa Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S. aliyechaguliwa kuwa Mkuu wa kwanza wa Kanda ya C.PP.S. Tanzania katika uchaguzi uliohitimishwa hivi karibuni. Itakumbukwa kwamba, kwa miaka mingi Padre Chesco Msaga amekuwa ni Makamu Askofu wa Jimbo la Dodoma, tangu wakati wa Askofu Mathias Joseph Isuja hadi Askofu mkuu Beatus Kinyaiya.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anakaza kusema, anamfahamu Padre Chesco Msaga kwani amekuwa ni msaidizi wake wa karibu. Ni kiongozi mchapakazi, mwenye busara, upeo na mang’amuzi mengi. Ni matumaini yake kwamba, ataliwezesha Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kukita mizizi yake katika maisha na utume wake. Anawaombea heri na baraka Wamissionari wote wa Damu Azizi ya Yesu katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.