2015-10-31 10:50:00

Utukufu wa Mungu ni mwanadamu aliye hai!


Tuanze mahubiri haya tukitafakarishwa na mafundisho ya Mtakatifu Ireneo – utukufu wa Mungu ni mwanadamu aliye hai. Mungu aliye hai ametuumba sisi ili tuwe hai. Hivyo kifo si mwisho wa maisha yetu. Mwisho wa maisha yetu hapa duniani ni mwanzo wa maisha mapya na Mungu. Ndivyo inavyotufundisha imani yetu. Tuongozwe na matumaini haya.

MWANADAMU; KKK 1008 na 413 tunasoma hivi; kifo ni tokeo la dhambi. Na kwamba mwanadamu ndiye asili ya mauti – kinyume cha muumba wake –Mwa. 3. Kifo cha kweli ni kifo cha mwenye dhambi. Mamlaka ya ufundishaji wa kanisa, mfafanuzi halisi wa matamshi ya Maandiko Matakatifu na mapokeo hufundisha kwamba kifo kimeingia ulimwenguni kwa sababu ya dhambi ya mwanadamu– Hek. 1,13 – yaani, Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea; Rom. 5,12. Ingawa mwanadamu ana hali ya kufa, Mungu alimweka asife. Kifo kilikuwa ni kinyume cha mipango ya Mungu Muumbaji, nacho kiliingia ulimwenguni kama tokeo la dhambi – Hek. 2,23-24. Kifo cha kimwili, ambacho mwanadamu angekuwa huru nacho, ndiye adui wa mwisho wa mwanadamu ambaye lazima kumshinda – 1Kor. 15,26 – adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.

MWILI – KKK 990 – neno mwili laeleza mtu katika hali yake ya udhaifu na ya kufa – Mwa. 6,3; Zab. 56,5; Isa. 40,6. Ufufuko wa mwili huonyesha kwamba baada ya kifo hakutakuwa na uzima wa roho peke yake bali kwamba hata miili yetu yenye hali ya kufa itapata tena uzima – Rom. 8,11 – lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.

KIFO - KKK 1006 – mbele ya kifo fumbo la hali ya kibinadamu linakuwa kubwa sana. Kwa namna moja kifo cha mwili ni kawaida, lakini kwa imani kwa kweli kifo ni mshahara wa dhambi – Rom. 6,23; - kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu, Mwa. 2,17 – walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. Kwa wale wanaokufa katika neema ya Kristo, kifo ni ushirika katika kifo cha Bwana, ili kuwezza kushiriki pia ufufuko wake.

Lakini kwa njia ya Kristo –tunapata uzima mpya – Rum. 8,29, - maana wale aliowajia tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu. 2Kor. 5,17, - hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. Yoh. 14, 5-6 – Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako, nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia na kweli na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Yoh. 3,5 – Yesu akajibu, amini, amini, nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Mk. 16,16 – aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa.

MAUTI NA UKOMBOZI.

Mtume Paulo anaelezea mauti na aina fulani ya ukombozi – Rum. 7,1…. Kwa kifo cha huyo mtu –tunakombolewa na maisha ya zamani – Rum. 7,1-5. – kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata tukaizalia mauti mazao. Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.

MAISHA YA MKRISTO – AINA MBILI ZA KIFO CHA MKRISTO.

Kwa njia ya ubatizo na imani –Rum. 1,6 – ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo -tumejiunga na Kristo aliyekufa na kufufuka – Rum. 8,11 – lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.

KKK 628 – ubatizo ambao alama yake ya asili na timilifu ni kuzamishwa, waashiria bayana kushuka kaburini kwa mkristo anayeifia dhambi pamoja na Kristo ili aishi maisha mapya. Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima – Rom. 6,4; Kol. 2,12 – mkazikwa pamoja naye katika ubatizo, na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu; Efe. 5,26.

Mauti ya pili – utengano wa mwili na roho hapa duniani.

Wafu wanafufuka namna gani? KKK 997 – kufufuka maana yake nini? Kwa kifo, mtengano wa roho na mwili, mwili wa mtu huoza, pindi roho yake huenda kukutana na Mungu ikingojea kuunganika na mwili uliotukuka. Mungu, kwa uwezo wake mkuu, atairudishia kwa hakika miili yetu, uzima usioharibika kwa kuiunganisha na roho zetu, kwa nguvu ya ufufuko wa Yesu. Rejea tena KKK – 1005 – ili kufufuka pamoja na Kristo, ni lazima kufa pamoja na Kristo; ni lazima kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana – 2Kor. 5,8 – lakini tunao moyo mkuu, nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana. Katika kwenda huko, yaani kifo, roho hutengana na mwili – Fil. 1,23. Nayo itaungana na mwili wake siku ya ufufuko wa wafu.

UFUFUKO

- KKK 999 – namna gani? Kristo amefufuka pamoja na mwili wake hasa – tazameni mikono yangu na miguu yangu ya kuwa ni Mimi mwenyewe. – Lk. 24,39, lakini hakuurudia uzima wa kidunia. Wakati huo huo ndani yake wote watafufuka pamoja na miili yao wenyewe waliyo nayo sasa, lakini mwili huo utageuzwa katika mwili mtukufu, katika mwili wa kiroho – Fil. 3,21; 1Kor. 15,44. labda mtu atasema – wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani? Ewe mpumbavu, uipandayo haihuiki isipokufa, nayo uipandayo hupandi mwili ule utakaokua ila chembe tupu … hupandwa katika uharibifu, hufufuliwa katika kutoharibika; wafu watafufuliwa wasiwe na uharibifu…maana sharti huu uharibikao, uvae kutoharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa – 1Kor. 15,35-53.

KKK – 998 –nani atafufuka? Watu wote waliokufa. Wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu - Yoh. 5,29; Dan. 12,2 –tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Mwadilifu, maana yake asiye na dhambi, afungamanaye na Mungu, hafi kabisa – Hek, 11,26 – lakini wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme Mkuu mpenda roho za watu, maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote.

Tutafakari tena na Mt. Ireneo –UTUKUFU WA MUNGU NI MWANADAMU ALIYE HAI. TAFAKARI KWA NINI KANISA HUADHIMISHA IBADA YA MISA YA MAZIKO YA MKRISTO? HUSALI MAKABURINI? IBADA YA MAZIKO: Ni adhimisho la Fumbo la Pasaka kwa matumaini. Ni sala ya kanisa – ili kuwaombea wale wote waliokwisha kuungana na mwili wa Kristo kwa njia ya ubatizo waingie katika uzima.  Ila kabla ya hapo – wapitie katika mauti kama Kristo Bwana wao alivyofanya, kwa sababu katika ubatizo walikufa pamoja na Kristo na kufufuka pamoja naye.

KUWAOMBEA MAREHEMU

Kanisa linawaombea marehemu ili watakaswe, ikiwa wanahitaji kutakaswa kabla ya kupokelewa mbinguni wakati miili yao inapobaki ardhini ikingoja kurudi kwa Kristo na ufufuko wa wafu.Hii ndiyo sababu kanisa linatolea sadaka ya misa kwa ajili ya marehemu. Pia kanisa linasali na kuwaombea marehemu kusudi wapate msaada wa kiroho na waamini walio bado hai wapate matumaini ya uzima ujao mbinguni.

UFUFUKO WA KRISTO – NI TOFAUTI NA UFUFUKO WETU.

Ufufuko wa Kristo ni tofauti na ufufuko mwingine – KKK 646 – ufufuko wa Kristo haukuwa kurudi katika maisha ya kidunia, kama ilivyokuwa ufufuko mwingine alioufanya kabla ya Pasaka; kama ule wa binti Yairo, wa kijana wa Naim, wa Lazaro. Kwa kweli hayo yalikuwa ni matokeo ya miujiza, lakini wale waiotendewa miujiza waliyarudia maisha ya kidunia ya kawaida. Wakati fulani watakufa tena. Ufufuko wa Kristo, kimsingi ni tofauti. Katika mwili wake uliofufuka, anapita kutoka hali ya kifo kufikia maisha mengine yaliyo juu ya wakati na mahali. Mwili wa Yesu katika ufufuko umejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu; unashiriki maisha ya uzima wa kimungu katika hali ya utukufu wake, hivi kwamba Mt. Paulo anaweza kusema kuwa Kristo ni Mtu Mbinguni – 1Kor. 15,35-50.

Tunasoma katika 1Thes. 4,14– maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa, akafufuka, vivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye na 1Kor. 15,20 – lakini sasa Kristo amefufuka toka wafu, limbuko lao waliolala. Kwa kifupi ufufuko wa wakristo wategemea ufufuko wa Kristo. Mungu Baba anawafufua wakristo kwa nguvu ile ile na karama ile ile aliyomfufua Yesu Kristo. Tunaamini kwamba mkristo amepewa uzima mpya unaomfanya kuwa mtoto wa Mungu – Rum. 8,14 – kwa kuwa wote wanaoongozwa na Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Mungu Baba huunganisha Kristo Mfufuka na mkristo kwa imani na ubatizo – Rum. 1,16; 6,4 – basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

HITIMISHO

1Kor. 2,6-10 – habari juu ya hekima ya Mungu – walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu, ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika, bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliazimu tangu milele, kwa utukufu wetu, ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja, maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu, lakini kama ilivyoandikwa; mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.