2015-10-30 14:21:00

Mwenyeheri Maria Theresa Casini alipenda kudumisha wito na utakatifu wa Mapadre


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 30 Oktoba 2015 anamtangaza Mtumishi wa Mungu Mama Maria Theresa Casini, Mwanzilishi wa Shirika Watumishi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kuwa Mwenyeheri, katika Ibada itakayoadhimishwa Jimboni Frascati, Roma, Italia. Ni Mama aliyejikita kuhakikisha kwamba anakuza na kudumisha wito wa maisha ya Kipadre, ili kuweza kulipatia Kanisa Mapadre wema, watakatifu na wachapa kazi, watakaojitosa kimasomaso kuwatangazia watu wa mataifa Habari Njema ya Wokovu.

Kutokana na kiu hii akaanzisha Seminari ndogo ya Marafiki wadogo wa Yesu, ili kukuza na kudumisha mbegu ya miito mitakatifu. Ni mama wa shoka, aliyejisadaka kwa ajili ya kuwahudumia Mapadre wazee, wagonjwa na maskini bila kuwasahau wale waliokumbana na mtikisiko wa imani katika maisha na utume wao wa Kipadre. Kimsingi Mama Maria Theresa Casini alitamani kuwaona Mapadre watakatifu wanaoambata utakatifu unaobubujika kutoka kwenye Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa, ili kuwakirimia waamini Sakramenti za Kanisa.

Kardinali Amato katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, Mwenyeheri mtarajiwa Maria Theresa Lutgarda Casini alizaliwa kunako tarehe 27 Oktoba 1864 katika familia iliyokuwa inaogelea katika umaskini mkubwa. Wazazi wake walikuwa ni wachamungu na wakarimu waliotaka kumwona mtoto wao akijikita katika maisha ya sala na matendo ya huruma hususan kwa maskini.

Malezi na makuzi haya yaliacha chapa ya kudumu katika akili na moyo wa Maria Theresa Lutgarda Casini, akaendelea kuwasaidia maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii katika hali ya ukimya na unyenyekevu pasi na kutaka makuu. Walipofariki wazazi wake, alipokelewa na kutunzwa na Padre Arsenio kwenye Abbasiya iliyoko Grottaferrata. Kunako mwaka 1894 kwa ruhusa ya Kardinali Serafino Vannutelli, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Frascati akaanza Shirika la Wateswa wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambalo leo hii linajulikana kama Shirika la Watumishi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Kardinali Amato anasema, changamoto endelevu ambayo imeachwa na Mwenyeheri Maria Theresa Casini ni kuendeleza dhamana na wito wa Shirika kwa kuwapokea na kuwasaidia : Majandokasisi, Mapadre na Maaskofu katika kutekeleza vyema utume na maisha yao ya Kikuhani; kwa kujikita katika utakatifu wa maisha unaorutubishwa kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu na kumwilishwa katika matendo ya huruma na sadaka. Huu ni mwaliko kwa Mapadre kuwa ni wapole, wanyenyekevu na wenye huruma, daima wajitahidi kumwiga Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.