2015-10-30 07:49:00

Mshikamano na umoja wa kitaifa ni muhimu sana katika kudumisha haki na amani!


Mama Kanisa anapenda kuutumia Mwezi Oktoba wa kila mwaka kuhamasisha ari na mwamko wa shughuli za kimissionari miongoni mwa Familia ya Mungu kwa kutambua kwamba, kila mwamini anaitwa na kutumwa na Kristo kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Waamini walei wanaweza kuitekeleza dhamana hii kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, yanayopania kuyatakatifuza malimwengu kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, hivi karibuni, limeadhimisha Kongamano la tatu la Kimissionari kitaifa kwa kukazia kwa namna ya pekee: haki, amani na upatanisho wa kitaifa, ili kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu unaogusa mahitaji ya mtiu mzima:kiroho na kimwili. Askofu mkuu Igantius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema, pasi na haki na amani, jitihada zote za maendeleo hazitaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Kongamano hili liliandaliwa na Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari nchini Nigeria, ili kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha haki, amani na upatanisho nchini Nigeria. Kongamano hili limewashikirisha wajumbe kutoka Familia ya Mungu nchini Nigeria. Imekuwa ni fursa ya kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa nchini Nigeria. Lengo ni kuimarisha majadiliano ya kidini, kisiasa na kijamii, ili kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa; amani na utulivu.

Katika miaka ya hivi karibuni, Nigeria imekuwa ni uwanja wa fujo na vurugu zinazoendeshwa na Kikundi cha Boko haramu ambacho kimepandikiza mbegu ya chuki, uhasama na vita miongoni mwa wananchi wa Nigeria. Vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini, vimesababisha mpasuko mkubwa na kinzani miongoni mwa wananchi wa Nigeria. Kanisa nchini Nigeria linapaswa kusonga mbele kwa imani na matumaini bila kukatishwa tamaa, kwani huu ni utume wake anasema Askofu mkuu Kaigama.

Nigeria ina watu wanaokaidiriwa kufikia millioni 160 na nusu ya wananchi hawa ni Wakristo na Waislam. Misimamo mikali ya kidini ni changamoto inayolitaka Kanisa kujikita katika majiundo makini ya mihimili ya Uinjilishaji, itakayojipambanua kwa kuwa na nyenzo makini za majadiliano ya kidini, ili watu waweze kuishi kwa amani na utulivu, huku wakiheshimiana na kuthaminiana na kwamba, tofauti zao za kidini, ziwe ni utajiri na amana ya maisha ya kiroho na wala si chanzo cha choko choko, kinzani na utengano wa kijamii.

Wananchi wa Nigeria wanapaswa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kuwa na mwelekeo finyu unaowagwa wananchi kwa misingi ya udini, usiokuwa na mvuto wala mashiko hata kidogo. Watu wawe na ujasiri wa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaopandikizwa kutokana na chuki za kidini. Inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya watu wanachezea maisha kwa kujitoa mhanga. Mchakato wa haki, amani, umoja na mshiamano wa kitaifa ni mambo msingi katika kupambana na umaskini na misimamo mikali ya kidini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.