2015-10-29 07:47:00

Wafundeni vijana kukumbatia utamaduni wa amani na utulivu!


Mama Kanisa daima amekuwa mstari wa mbele kuwafunda walimwengu kuhusu umuhimu wa kuchuchumilia na kuambata amani katika maisha yao, kama chachu muhimu sana katika maendeleo ya watu kiroho na kimwili. Waamini na wapenda amani wanayo dhamana kubwa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kuhusu umuhimu wa amani katika maisha bila kuchoka kwani amani inawezekana kabisa ikiwa kama binadamu watapania.

Huu ni mchango ambao umetolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatano tarehe 28 Oktoba 2015 kwenye Kongamano la kimataifa kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipotoa Tamko kuhusu majadiliano ya kidini “Nostra Aetate” na waamini wa dini mbali mbali duniani. Kongamano hili la siku mbili kuanzia tarehe 26 hadi 28 Oktoba liliandaliwa na Mabaraza ya Kipapa ya majadiliano ya kidini, Baraza la Kipapa la uhamasishahi wa umoja wa Wakristo pamoja, Tume ya Kipapa ya mahusiano na Wayahudi pamoja na Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma.

Kongamano hili limehudhuriwa na waamini kutoka katika dini mbali mbali ambao kwa pamoja wanapania kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano, haki na amani. Wajumbe hawa walibahatika kushiriki katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumatano iliyojikita katika Jubilei ya miaka 50 ya Majadiliano ya kidini kati ya Kanisa Katoliki na dini mbali mbali duniani, lakini kwa namna ya pekee, kati ya Wakristo, Waislam na Wayahudi.

Kardinali Parolin katika tafakari yake kwa ajili ya kufunga kongamano hili la kimataifa amajielekeza zaidi katika elimu ya amani, kwa kuangalia amani katika mwelekeo mpana zaidi, amani kadiri ya Maandiko Matakatifu, amani kama wanavyofundisha viongozi wa Kanisa katika kipindi cha miaka hamsini iliyiopita na umuhimu wa majiundo makini ya amani kwa watu wa nyakati hizi kwa kutambua kwamba vita imekuwa ni mama wa umaskini na chanzo cha majanga na maafa makubwa kwa binadamu.

Amani ni fadhila inayowezekana ikiwa kama haki msingi za binadamu zitapewa kipaumbele cha kwanza sanjari na kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano miongoni mwa watu. Shalom, ni neno linalomaanisha ustawi, amani, baraka na linaonesha ukuu wa Mungu unaopaswa kukumbatiwa kwa uaminifu mkubwa. Amani ni zawadi na baraka kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowajibisha binadamu na kwamba amani kadiri ya Agano Jipya ni Kristo mwenyewe, kielelezo cha uwepo wa ufalme wa Mungu unaojikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano.

Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, viongozi wakuu wa Kanisa wamekita mafundisho yao juu ya amani, lakini kwa namna ya pekee kabisa Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa kitume, Amani Duniani, Pacem in Terris anayekazia umuhimu wa haki, uhuru, ukweli, upendo na msamaha kama mambo msingi ya kujenga na kudumisha amani duniani sanjari na kukuza mahusiano mema kati ya wananchi na viongozi wao, Jumuiya za kisiasa na ulimwengu katika ujumla wake.

Haki asilia na kanuni maadili zinapaswa kuzingatiwa na wote, ili kweli amani iweze kutawala katika mioyo ya watu. Ikiwa kama kanuni hizi msingi zingefuatwa na kuzingatiwa anasema Kardinali Pietro Parolin, Jumuiya ya Kimataifa isingeshuhudia wala kuendelea kushuhudia mauaji ya kimbari sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, dunia kwa sasa inaanza kuonja cheche za Vita kuu ya tatu ya dunia. Hii inatokana na ukweli kwamba, rasilimali na utajiri wa mali asili, uchu wa mali na madaraka, udini na utaifa ni mambo ambayo yameendelea kuwa ni chanzo kikuu cha vita na matokeo yake ni makundi makubwa ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi kuendelea kuteseka kwa kutafuta hifadhi na usalama wa maisha.

Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mwaliko kwa waamini kuchuchumilia: haki msingi za binadamu, amani, ustawi na maendeleo ya binadamu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Majadiliano ya kidini yanalenga kujenga na kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano kati ya walimwengu. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea amani duniani, kila tarehe mosi, Januari yaliyoanzishwa na Mwenyeheri Paulo VI ni changamoto endelevu kwa waamini kusali kwa ajili ya kuombea amani na Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujikita katuika mchakato wa kudumisha utamaduni wa amani.

Majiundo makini ya amani yanapaswa kujikita katika dhana ya majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na upatanisho kama anavyokaza kusema Mwenyeheri Paulo VI. Mtakatifu Yohane Paulo II alifanikiwa kuwakutanisha viongozi wa dini mbali mbali ili kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Assisi tarehe 26 Oktoba, 1986. Papa mstaafu Benedikto XVI alikazia umuhimu wa vijana kufundwa utamaduni wa haki na amani na kwamba, majadiliano ya kidugu ni muhimu sana katika kukuza haki, amani na mshikamano wa kidugu.

Katika nyakati hizi, Mama Kanisa anapenda kuwahamasisha waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuwekeza katika utamaduni wa amani kwa kuwa na lugha inayowagusa vijana wa kizazi kipya kama chachu ya maendeleo endelevu. Utamaduni wa amani utoe kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; haki msingi za binadamu na vipaumbele vyake: kiroho na kimwili. Kila mtu ajisikie kwamba, anapenda na kupendwa na watu. Majiundo ya utamaduni wa amani yajikite pia kwenye mitandao ya kijami inayotumiwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa kizazi kipya. Watu wajifunze kupenda na kuheshimu tofauti zao; uhuru wa mtu kutoa mawazo yake sanjari na kujenga utamaduni wa kusikilizana.

Kardinali Pietro Parolin anakazia kwa kusema kwamba, majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; utu na heshima ya binadamu ni mambo muhimu sana katika kukuza na kudumisha utamaduni wa amani na kwamba, amani ni fadhila na zawadi kubwa kutoka kwa Mungu inawezekana, ikiwa kama kila mtu atatekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.