2015-10-26 15:05:00

Kanisa litaendelea kuonesha mshikamano wa dhati na Wakristo Mashariki ya Kati!


Waamini pamoja na wananchi wote wa Iraq na Syria wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na vita na kinzani zinazoendelea katika nchi hizi. Kanisa linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wale wote wanaoteseka na kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu yatasaidia kuganga madonda ya vita pamoja na kufuta machozi ya watu wasiokuwa na hatia wanaoendelea kuteseka kutoka na vita; hususan wakati huu ambapo mtutu wa bunduki unaonekana kutawala dhidi hata ya nguvu ya sala.

Maeneo ya Mashariki ya kati yanaendelea kuathirika kutokana na chuki, misimamo mikali ya kidini, vitendo vya kigaidi, nyanyaso na dhuluma za kidini zinazopelekea maelfu ya watu kuzikimbia nchi zao sanjari na kung’olewa katika mapokeo. Hapa walengwa wakuu ni Wakristo huko Mashariki ya Kati, mahali ambapo Mzee Ibrahimu alianzia safari yake ya imani; sauti ya Manabii isikike tena, kuwatangazia matumaini watu wote walioko uhamishoni; ili kweli damu ya mashuhuda wa Injili, isaidie kujenga na kukuza amani na utulivu miongoni mwa Wakristo na Waislam. Kwa bahati mbaya dhuluma imeendelea kushika kasi kiasi hata cha kuzalisha mashuhuda wa imani.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Sinodi ya Kanisa la Wakristo wa Caldea, Jumatatu tarehe 26 Oktoba 2015. Watu wana hamu ya kutaka kubaki katika maeneo yao na kwamba, Vatican na Kanisa katika ujumla wake litaendelea kushikamana na Wakristo huko Mashariki ya Kati, ili kudumisha Mapokeo ya Kikristo wanayobeba mabegani mwao. Hii ni changamoto kwa Maaskofu na viongozi wa Kanisa kuwa ni vyombo na wajenzi wa umoja, majadiliano na ushirikiano kati ya watu katika maisha ya hadhara, ili kuponya na kuganga madonda ya utengano.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kwa mara nyingine tena kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kuleta amani ya kudumu katika maeneo ambayo kwa sasa yamegubikwa na vita na chuki, ili upendo, haki na amani viweze kutawala tena.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Sinodi wanayoendelea kuadhimisha hapa mjini Roma ni safari inayowawezesha kutembea pamoja katika umoja na utofauti; kwa kujengana na kuimarishana kidugu, daima wakimwangalia Kristo mchungaji mwema. Sinodi ni dhana ngumu katika utekelezaji wake, kwa kutambua kwamba, uongozi kwa Kanisa ni huduma, kiini cha Fumbo la Kanisa. Maaskofu wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutenda yote katika: huruma, unyenyekevu, uvumilivu na ukarimu; mambo yanayojenga na kudumisha umoja.

Maadhimisho ya Sinodi yajenge na kuimarisha uwajibikaji, ushiriki na huduma mintarafu dira na mwongozo wa Yesu Kristo mchungaji mwema, anayejitaabisha kumtafuta na kumhudumia Kondoo aliyepotea. Maaskofu wawe mstari wa mbele kuwatafuta waamini, watawa na wakleri wanaolegea katika imani kwa kutambua kwamba, wao wenyewe wanapaswa kujisadaka, ili kuweza kutekeleza dhamana hii katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu waoneshe upendo na heshima ya Kibaba kwa Wakleri wao ambao kimsingi ni wasaidizi wao wa kwanza katika mchakato wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu; wajitahidi kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa waamini tayari kutafuta suluhu ya pamoja kuhusiana na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni anawataka wajumbe wa Sinodi ya Kanisa la Wacaldea kutekeleza dhamana na utume wao kwa kujikita katika moyo wa umoja unaosimikwa katika udugu; kwa kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimissionari, ili kuwasha moto wa mapendo kwa familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.