2015-10-20 12:06:00

C.PP.S endelezeni utume wa kimissionari kwa ari na moyo mkuu!


Katika kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, zilizofanyika Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania, Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro aliwataka Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania ambayo ni matunda ya maadhimisho haya kuthubutu kuiendeleza kazi na utume wa kimissionari ndani na nje ya Tanzania, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu. Daima wahakikishe kwamba, wanamshirikisha Mwenyezi Mungu katika dira na mipango na mikakati ya maisha ya kitume na kimissionari.

Miaka 50 ya Uwepo wa Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania, ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Hii ni changamoto kwa Kanisa la Tanzania katika ujumla wake kuhakikisha kwamba, linaliendeleza Shirika kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho! Hii ni zawadi na amana kubwa kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, kumbe ni jukumu la Wamissionari wakisaidiana na Maaskofu kuliendeleza zaidi, huku wakithubutu kuboresha yale waliorithi pamoja na kuanza mapya kadiri Roho Mtakatifu atakavyowaongoza.

Jubilei ni kipindi cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu na wakati muafaka wa kujiwekea mikakati na dira za shughuli za kichungaji kwa siku za usoni. Kanisa nchini Tanzania, hapo mwaka 2018 litaadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania, itakuwa ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa wema na tunza yake ya kibaba kwa Kanisa nchini Tanzania.

Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu Mtakatifu Gaspar del Bufalo alipoanzisha Shirika ya Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu yamefikia kilele chake tarehe 15 Agosti 2015. Nchini Tanzania maadhimisho haya yaliongozwa na kauli mbiu “Tushirikishane tone la upendo”. Maneno yaliyomo kwenye kauli mbiu hii yamewafikirisha sana waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Tanzania. Hii inatokana na ukweli kwamba, Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu unaoambata kazi ya Ukombozi.

Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogo alikuwa ni mlezi wa maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, nchini Tanzania. Jimbo Katoliki Dodoma halikuwa na Askofu kwa wakati huo! Kilele cha Ibada ya Misa Takatifu kiliongozwa na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Dodoma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.