2015-10-18 11:55:00

Jikiteni katika upendo na huduma; kataeni kishawishi cha uchu wa madaraka!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 18 Oktoba 2015 katika Maadhimisho ya Siku ya 89 ya Kimissionari Ulimwengu amewatangaza Wenyeheri: Vincenzo Gross, Padre Mwanzilishi wa Shirika la Mabinti wa Vituo vya michezo “Oratorio”; Sista Maria wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, mkuu wa Shirika la na Watawa Waambata Msalaba; Mwenyeheri Ludovico Martin, Mwamini mlei na Baba wa familia pamoja na mke wake Maria Azelia Guèrin, kuwa watakatifu. Ibada hii imefanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya ishirini na tisa ya Mwaka B wa Kanisa inamwonesha Mtumishi wa Mungu, asiyekuwa na makuu, aliyeteswa, akanyanyaswa na kutengwa na hatimaye kufa kifo cha aibu, lakini katika hali ya ukimya na unyenyekevu mkubwa akaweza kutekeleza utume na kazi ya ukombozi kwa mwanadamu wengi. Ni mateso, kifo na ufufuko wake uliowezesha ukombozi na mchakato wa upatanisho kati ya Mungu na binadamu.

Akizungumzia kuhusu uongozi kama huduma, Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu aliwakemea mitume wake waliokuwa na mwono tenge kuhusu uongozi, kwa kuwakumbusha kwamba, katika maisha na utume wao, watashiriki pia Kikombe cha mateso, lakini haikuwa kazi yake kuwapatia nafasi ya kukaa kuume au kushoto katika Ufalme wa Mungu, mwaliko wa kuambata njia ya upendo na huduma badala ya kukumbatia kishawishi cha uchu wa madaraka, ili kuwatala wengine kwa fimbo ya chuma!

Baba Mtakatifu anasisitizia kwamba, wakati ambapo kuna uchu wa mali na madaraka katika ulimwengu mamboleo, wafuasi wa Kristo wanapaswa kujikita katika huduma inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu badala ya uchu wa madaraka unaotaka kuwatawala wengine kwa mabavu! Anakumbusha kwamba, Mwana wa mtu ni yule ambaye atapokea nguvu, furaha na ufalme, hali inayomwonesha Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyetwaa mwili kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa binadamu, akadiriki kuchukua nafasi ya mwisho, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utumishi ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza kwamba, kuna tofauti kubwa kati ya sifa za uongozi kadiri ya vionjo vya walimwengu na uongozi kadiri mafundisho na mfano wa maisha ya Yesu. Uongozi kadiri ya walimwengu unafumbatwa katika uchu wa madaraka, heshima, mafanikio, chuki, lakini uongozi kadiri ya Kristo ni kuubeba Msalaba, tayari kuteseka kama kielelezo cha mshikamano wa upendo; Ukuhani unaojikita katika huruma na upendo, kwani Yesu anatambua fika madhaifu na mapungufu ya binadamu na anawataka kutambua dhambi na madhara yake.

Utukufu wa Yesu unaojionesha kwa namna ya pekee katika upendo, mshikamano, ili kuwakirimia rehema na neema inayoganga, inayoponya na kumsindikiza mwanadamu katika shida na mahangaiko yake ya ndani. Wakristo kwa njia ya Ubatizo, wanashiriki pia ukuhani wa Kristo, wamepokea upendo unaobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu, changamoto ya kuwa kweli ni mifereji ya upendo na huruma, hususan kwa wale wanaoteseka, wapweke na waliokata tamaa.

Watakatifu waliotangazwa na Mama Kanisa ni waamini waliojipambanua kwa njia ya huduma inayojikita katika unyenyekevu na upendo, huku wakijitahidi kumuiga Kristo Bwana na Mwalimu. Mtakatifu Vincenzo Grossi alikuwa ni Paroko mahiri, aliyeguswa na shida za watu wake hususan mahangaiko ya vijana. Alijitahidi kuwamegea wote Mkate wa Neno la Mungu, akawa Msamaria mwema kwa wenye shida.

Sista Maria wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, alionesha kwa namna ya pekee uongozi unaojikita katika huduma, akatoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto wa maskini na wagonjwa. Watakatifu Ludovico Martin na mke wake Maria Azelia walijitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa familia, kwa kujenga mazingira ya imani na upendo na matunda ya kazi hii ni Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. Ushuhuda wa watakatifu ni kielelezo cha huduma ya furaha kwa jirani inayojiaminisha katika msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Huko mbinguni, waendelee kuiombea Familia ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.