2015-10-17 15:21:00

Sinodi za Maaskofu zimeliwezesha Kanisa kutembea katika umoja na mshikamano


Jubilei ya miaka hamsini tangu kuanzishwa kwa Sinodi za Maaskofu ni mchakato ambao umeliwezesha Kanisa kuonja uzuri na umuhimu wa kutembea na kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano na kwamba, huu ni urithi mkubwa kutoka kwa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto ya kuendeleza moyo na mbinu ya maadhimisho haya kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Maadhimisho ya Sinodi yanaweza kuboreshwa zaidi kwa kusoma alama za nyakati; kwa kupenda na kutumikia katika utekelezaji wa utume wa Kanisa, licha ya tofauti na kinzani zinazoweza kujitokeza.

Maadhimisho ya Sinodi ni hija ya maisha ya Kanisa ambayo Mwenyezi Mungu anataka kwa ajili ya Kanisa lake katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulipoanzisha maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu. Sinodi ni hija ya watu wa Mungu wanaotembea katika umoja unaojionesha hata katika tofauti zao, ili kuunda Ukuhani mtakatifu wa watu wa Mungu waliopakwa mafuta na Roho Mtakatifu.

Maadhimisho ya Sinodi ni kielelezo cha imani na maadili ya Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu. Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linaihusisha kikamilifu familia ya Mungu kabala, wakati na baada ya maadhimisho ya Sinodi ili kuonesha ile furaha, matumaini, machungu na magumu wanayokabiliana nayo katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Kanisa lijenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kutambua kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kwa Kanisa. Kwa mantiki hii, Sinodi ni mahali pa kwanza kabisa pa kusikiliza na kusikilizana, kwa kushiriki katika ile sauti ya kinabii kutoka kwa Kristo. Sinodi ni mahali pa kusikiliza shuhuda mbali mbali kutoka kwa Familia ya Mungu na hatimaye, kumsikiliza Khalifa wa Mtakatifu Petro, mchungaji mkuu na mwalimu wa Wakristo wote; dhana inayodai kwanza kabisa utii kadiri ya sheria za Kanisa, mapenzi ya Mungu pamoja na Mapokeo ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, maadhimisho ya Sinodi yanatekelezwa chini ya usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi ni fursa makini katika kufahamu maana ya Uongozi wa Kanisa, kwani Kanisa na Sinodi ni sawa na chanda na pete, dhana zinazotegemeana katika hija ya pamoja, ili kukutana na Yesu Kristo katika hali ya unyenyekevu.

Yesu alianzisha Kanisa na kuliweka chini ya usimamizi wa Mitume na Mtakatifu Petro akateuliwa kuwa ni kiongozi mkuu, mwamba thabiti ambao utakuwa na dhamana ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani; viongozi wa Kanisa waoneshe fadhila ya unyenyekevu katika huduma yao kwa waamini ambao wamekabidhiwa kwao na Kristo Yesu. Hii ni huduma ya upendo kama Yesu mwenyewe alivyofanya kwa kuwaosha miguu mitume wake. Uongozi ni huduma na madaraka yanajikita katika nguvu ya Msalaba. Sinodi za Maaskofu ni muhimu sana ili kuweza kutoa maamuzi katika maisha na utume wa Kanisa, kwani hapa kuna ushirika mpana zaidi kadiri ya Sheria za Kanisa, hali inayoonesha mshikamano wa dhati wa Familia ya Mungu inayotembea kwa pamoja.

Mchango wa wadau mbali mbali kutoka katika Makanisa mahalia; Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu na hatimaye mchango wa Kanisa la Kiulimwengu unaowajumuisha Maaskofu, wajumbe pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro unapaswa kuzingatiwa, ili kweli matunda ya Sinodi yaweze kuonekana ili Familia ya Mungu iweze kuguswa! Maadhimisho ya Sinodi ni kipaumbele cha kwanza kinachopaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Kwa njia hii, majadiliano na mahusiano ya kiekumene na Makanisa mengine yataweza kuboreka zaidi na hivyo kumpatia Khalifa wa Mtakatifu Petro mwanga na mang’amuzi makubwa katika kuliongoza Kanisa la Kristo, kielelezo cha umoja na upendo. Hapa kuna haja ya kuwa na mageuzi makubwa kuhusu dhana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Kanisa.

Ikumbukwe kwamba, Kanisa linalojikita katika dhana ya Sinodi ni kielelezo cha ushirikishwaji wa familia ya Mungu kwa njia ya mshikamano, ukweli na utunzaji wa mali ya umma, badala ya rasilimali ya nchi kuwekwa chini ya usimamizi wa watu wachache wenye madaraka makubwa. Wananchi wanapaswa kushirikishwa ili kukuza na kudumisha utu na heshima yao; huduma sanjari na kukuza pamoja na kuimarisha haki katika udugu, kwa kujenga dunia bora zaidi kuliko ilivyo kwa sasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.