2015-10-16 15:41:00

Utume wa familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo! Yataka moyo!


Mababa wa Sinodi ya familia wamehitimisha tafakari za makundi madogo madogo na sasa wanaelekeza nguvu zao katika sehemu ya tatu ya hati ya kutendea kazi inayojikita katika utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Mababa wa Sinodi wamejadili kwa kina na mapana kuhusu ukarimu kama sehemu ya utambulisho wa familia za Kikristo, kwa kuwasaidia watoto na watu wanaoishi katika mazingira magumu. Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao. Shauku ya kutaka kupata mtoto kwa gharama yoyote ile ni kielelezo cha ubinafsi hali ambayo inapelekea baadhi ya wanandoa kutafuta watoto wanaozaliwa kwa njia ya chupa au kwa mimba za kupangisha.

Misigano na talaka katika maisha ya ndoa ni kielelezo cha ukosefu wa ukomavu wa imani na kimaadili, lakini kwa upande mwingine ni ushuhuda kwamba, pengine wanandoa hawakupata maandalizi ya kutosha kabla ya kuamua kufunga ndoa, utume ambao una madai na haki zake. Ili kupata wanandoa wadumifu kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anawafunda vyema Wakleri watakaowasaidia wanandoa katika hija ya maisha yao, kwa kujitahidi kusoma alama za nyakati, huku wakiongozwa na jicho la Msamaria mwema na mwenye huruma kwa jirani zake. Huu ni mwaliko wa kuwapokea na kuanza mchakato wa kuwapatia tiba muafaka kadiri ya mafundisho ya Kanisa, ushuhuda makini, tafakari na maisha ya sala.

Ili Wakleri waweze kutekeleza vyema dhamana hii kuna haja ya kuwapatia majiundo makini katika maisha ya Ndoa na familia, ili kuonesha uwepo wa karibu wa Kanisa kwa familia, hususan zenye kinzani na migogoro ya kifamilia. Wakleri wafahamu sheria, mafundisho na Sakramenti za Kanisa ili kutoa majibu muafaka kadiri ya matatizo yanayojitokeza. Toba, wongofu wa ndani na imani thabiti ni muhimu sana kwa wanandoa wenye kinzani za maisha ya kifamilia wanaotaka kupokea Ekaristi Takatifu. Lakini pia wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa masikitiko makubwa Mababa wa Sinodi wamegusia tatizo la uchumba sugu ambalo limeenea katika mifumo mbali mbali. Kimsingi mwanadamu ana kiu ya kutaka kuunda familia, lakini wakati mwingine anakosa ujasiri wa kufanya maamuzi magumu katika maisha kutokana na sababu mbali mbali. Mababa wa Sinodi wamegusia pia tatizo la wahamiaji na wakimbizi; sheria na vizingiti wanapotaka kuoa au kuolewa. Kuna haja ya Kanisa kupata suluhu ya kudumu, ili kuwasaidia wahamiaji na wakimbizi kutokengeuka na kupoteza dira na mwelekeo wa imani yao kutokana na masuala ya ndoa na familia.

Ndoa za watu wa jinsia moja zinazoendelea kupigiwa debe kwa kutungiwa sheria na nchi mbali mbali duniani, limegusiwa pia. Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, hapa haki msingi, ustawi na maendeleo ya watoto wadogo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Watoto wanahaki ya kuwa na mama na baba watakaowasaidia katika malezi na makuzi yao. Shule na taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, zipewe haki na dhamana ya kuendelea kutangaza Injili ya familia, maadili na utu wema. Kuna haja ya kuangalia mikakati ya kichungaji ili kuwasaidia waamini wenye mielekeo ya ndoa za jinsia moja. Waamini wanachangamotishwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Wanawake walindwe na kuthaminiwa dhidi ya vipigo na nyanyaso za majumbani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wanaendelea kusali kwa ajili ya kuombea maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Kitubio kwa ajili ya wanandoa waliotalakiana na kuamua kuoa au kuoana tena, zimejadiliwa mintarafu dhana ya dhambi na kwamba, wanaopenda kupatiwa tena huduma hii na Mama Kanisa watambue dhambi hii, kwa kujuta na kuinua kutoitenda tena, ili kuanza hija ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata msamaha, huruma na upendo wa Mungu.

Kanisa linapenda kuwakumbatia wote na kwamba, Yesu Kristo ameteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu katika lindi la dhambi na mauti. Waamini wanaoogelea katika dhambi, waonjeshwe upendo, ili waweze kutubu, wasaidiwe kuanza mchakato wa upatanisho, ili kupokea huruma ya Mungu. Wanandoa wanaoishi katika mgogoro wa maisha ya kifamilia wawe makini, ili kamwe wasiwe ni sababu ya kashfa kwa waamini wengine.

Ekaristi Takatifu ina thamani kubwa katika hija ya ukombozi wa mwanadamu. Kanisa lijitahidi kutoa mafundisho makini, ili kuimarisha na kukuza Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Sakramenti za Kanisa. Waamini wajenge mahusiano ya karibu zaidi na Yesu Kristo kwa njia ya Neno la Mungu, Sala na Sakramenti za Kanisa. Wanandoa watambue kwamba, Sakramenti ya Ndoa takatifu inawakirimia furaha na matumaini katika maisha yao, wanandoa wafundwe na kupatiwa Katekesi ya kina, ili kufumbata na kuambata Injili ya Uhai kwa kujikita katika mpango wa uzazi kwa njia asili. Utu, haki na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza.

Mababa wa Sinodi wamegusia pia athari za mashambulizi ya kigaidi yanayoharibu mafungamano, ustawi na maendeleo ya kijami. Tatizo la watoto wadogo ambao wanajikuta katika makundi ya wahamiaji pasi na uangalizi wa wazazi au walezi wao; biashara ya ukahaba na ngono; ni mambo yanayohitaji kushughulikiwa kikamilifu pamoja na kupata mshikamano kutoka kwa Kanisa. Sinodi imemkumbuka kwa namna ya pekee Mtakatifu Yohane XXIII aliyezindua maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, aliyekazia huruma ya Mungu katika kuganga na kuponya madonda ya Watoto wa Mungu na kwamba, amani ipewe msukumo wa pekee katika maisha ya kijami.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.