2015-10-15 16:05:00

Bwana, tupe shavu! Msalaba baadaye! Mpasuko kwa kuwania madaraka!


Tunasikia mara nyingi kuwa kuna mpasuko ndani ya chama fulani cha siasa. Viongozi wanatofautiana fikra na kusambaratika. Wanachama wakongwe wanajitoa kabisa uanachama na pengine wanajiunga au kuanzisha chama kingine. Mpasuko unaweza pia kutokea ndani ya dini yoyote ile au hata ndani ya taifa lililoungana. Leo tutaushuhudia mpasuko wa kutisha ndani ya chama fulani tawala. Kumetokea mtafaruku ndani ya chama na wanachama wake wamechafuana nyongo vibaya sana na kugawanyika. Ili uweze kuelewa zaidi yaliyojili katika mpasuko huo, fuatilia kwanza mambo yaliyotokea katika Injili ya leo.

Yesu akiwa katika harakati zake za kutembea huku na kule, wanafunzi wake wakawa wanazifuatilia nyendo zake na kujaribu kuiga sera zake. Wakati mwingine walimwelewa lakini wakati mwingine hawakumwelewa kabisa hadi kupata hata woga na hofu kutokana na lugha zake hasa anapowaambia anaenda kuteswa. Kumbe watu wengine waliokuwa wanamfuata hasa vijana kwa vile walikuwa wanalishwa mikate na pengine wanaponywa magonjwa yao walikuwa wanamfuata kwa ushabiki tu bila kumwelewa. Hata mitume wengine walimwelewa jinsi wanavyotaka wao kuelewa hasa pale alipowaambia kuwa: “Mwana wa mtu atatolewa kwa makuhani wakuu.”

Kwa bahati mbaya neno “atatolewa” halieleweki na wengi tunadhani kuwa “atatolewa” na Yuda. Kumbe ukweli ni kwamba jina la mtendaji limefichwa halitajwi kwa sababu ya heshima. Neno hili “atatolewa” linamhusu Mungu. Yeye mwenyewe ndiye atamkabidhi Mwanaye mikononi mwa binadamu. Mungu aliweza kufanya hivyo, kwa vile ulimwengu wa kale haukuwa tena wa kiutu bali wa kiumbwa mwitu. Kwani viongozi wake walikuwa kama wanyama wakali wanaowaburuza raia wao. Akawaambia mitume wake: “Ninawatuma kama mwanakondoo kati ya mbwa mwitu.” Yesu anaorodhesha matendo saba ya nguvu za ulimwengu wa kinyama ambazo Mwana wa mtu atakabiliana nazo. Mosi, Mwana wa mtu atatolewa kwa wapagani; Pili, atakabidhiwa kwa mamlaka ya viongozi wa nchi; Tatu watamdhihaki; Nne, watamtemea mate, Tano, watampiga mijeledi; Sita, watamwua; Saba, baada ya siku tatu atafufuka. Matendo sita ya mwanzo ni ya binadamu lakini tendo la saba ni la Mungu pekee yake, yaani ufufuo.

Mitume waliposikia kuwa ametamka mara tatu kwenda Yerusalemu kuteswa lakini hatimaye katika utukufu, wanafunzi wawili Yakobo na Yohane wana wa Zebedeo wanajitosa kumweleza Yesu ndoto zao wakiwania zaidi kuupata utukufu. Wanafunzi hao wanamwambia Yesu: “Mwalimu, twataka utufanyie lolote tutakalokuomba.” Hapa tendo hili “twataka” limefasiriwa vizuri kutoka lugha ya Kigiriki thelomen yaani mwalimu afuate matakwa yao. Lakini Yesu anawajibu kwa kuwauliza kama wafanyavyo Marabi ili jibu litoke nafsini mwao wenyewe: “Mwataka niwafanyie nini? Wakamwambia, “utujalie sisi tuketi mmoja mkono wako wa kuume na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.”

Neno hili “utukufu” kwa Kiebrania linamaanisha uzito kama uzito wa ngano tofauti na makapi yanayopeperushwa na upepo kama asemavyo mzaburi:  “Maisha ya mwenye haki ni kama ngano na maisha ya wasio haki ni kama makapi yanapeperushwa na upepo.” (zaburi 1:4) “Utukufu” ni uzito au hadhi atakayokuwa nayo Yesu atakapoingia ikulu na kuketi katika kigoda chake. Ikumbukwe kuwa  wanafunzi hawa wawili walishakuwa maarufu sana katika kikundi kile cha mitume. Ndiyo walioitwa Boanerge yaani “Wana wa Ngurumo” au “wana wa radi.” Kutokana na heshima na umaarufu waliokuwa nayo mitume hawa wawili, Luka haandiki habari hii ya kutaka ukuu asije akawavunjia heshima.

Mwinjili Matayo anapindisha kidogo maelezo akisema kwamba alikuwa mama yao ndiye aliyewaombea wanae fursa hiyo. (Mt 20:20-21) Marko anapoiandika Injili hii Yakobo alishafariki tayari lakini ndugu yake Yohane alikuwa bado anaishi na kuheshimika sana. Aidha likuwa imeshapita miaka minne tangu yatokee madhulumu ya Nero huko Roma. Kwa hiyo habari hi inawalenga waumini waliobaki ambao baada ya madhulumu walijisikia kuwa wa pekee wakabaki kuwania kupewa nafasi za kwanza kama wanachama waanzilishi wa Ukristo.

Yesu anawaambia wanafunzi wale: “Ninyi hamuelewi mnachokitaka. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?” Kikombe (kalisi) na ubatizo ni picha mbili za hatima ya maisha ya Yesu. Kunywa kikombe kimoja ni sawa na kushirikiana au kuwa na hatima moja. Ubatizo ni kuzamishwa majini sawa na kuingia kaburini. Kwa hiyo kushiriki utukufu (kuwa mzito kadiri ya Yesu) maana yake kushiriki kidhati hatima  yake ya kutoa maisha. Mitume hao wanataka mabadiliko hivi wanajibu mara moja bila kufikiri kwani wakijua kwamba Bwana wao akiingia tu ikulu nao wataingizana pamoja naye kupanda vyeo.

Yesu anaheshimu kutoelewa kwao mambo kwani anajua itakuja siku wataelewa kwa vitendo. Ndiyo maana anawajibu, “lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa,” Kwamba utukufu (uzito) wa Mungu hauko katika kutumikiwa na binadamu, bali ni Mungu ndiye anayemtumikia binadamu. Kwa hiyo unaona tofauti kati ya utukufu (wazito) wa ulimwengu huu na utukufu (uzito) wa Yesu. Uzito au utukufu wa ulimwengu huu ni kutawala na kukandamiza wengine; ni kupata vyeo na sifa; ni kumiliki na kujilimbikiza mali; Kumbe, utukufu (uzito) wa Yesu ni kutumikia, ni kushuka, ni  kugawa mali yote na kujenga huduma ya upendo kwa Mungu na jirani.

Baada ya kurushiana lugha hii, ndiyo unatokea mpasuko mkali katika kikundi hiki cha Wanachama kumi na wawili: “Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohane”(10:41). Neno hili kukasirika linamaanisha mgomo, maasi, kutoelewana, mgawanyiko, mpasuko. Huu ndiyo mpasuko wa kwanza katika historia ya kanisa uliosababishwa na kuwania utukufu, uzito, ukuu au cheo. Mpasuko huu wa mitume wawili dhidi ya kumi, unaturejesha moja kwa moja kwenye mpasuko ule wa makabila kumi na mawili ya waisraeli. Taifa hilo lilipasuka pande mbili likiyagawa makabila kumi ya ufalme wa kaskazini na makabila mawili ya ufalme wa kusini mara baada ya kufa Mfalme Sulemani.

Chokochoko ilianza katika makabila haya kumi na mawili, pale Yeroboamu (Mwana wa Sulemani) alipoenda Shekemu (kaskazini) ili kunadisha sera zake na kujitambulisha kama mfalme mrithi wa makabila yote ya kaskazini na kusini ya taifa la Israeli. Yeroboamu alianza kwa kuomba maoni toka kwa wazee na vijana kabla ya kushika dola. Wazee wa makabila kumi ya kaskazini wakamwambia kwamba wao hawana tatizo, wako tayari kuwa chini ya himaya yake, lakini wakamwonya asiwe fisadi kama Baba yake Sulemani aliyewakandamiza sana kwa kuwatoza ushuru na kodi kubwa ili kuwahudumia masulia wake wengi aliokuwa anakaa nao kwenye ikulu (I Wafal. 12:4).

Baada ya wazee akaenda pia kusikiliza maoni ya vijana wa makabila mawili ya kusini, nadhani ni wale aliokuwa nao kijiweni wakati baba yake anatawala. Hao  wakamwambia sisi bwana tunataka kuendelea kufaidi maisha pamoja na wewe, kwa hiyo kodi ziendelee mtindo mmoja. “Naye Sulemani akaliacha shauri la wazee, walilompa akataka ushauri kwa wale vijana waliokuwa pamoja naye na kusimama mbele yake.” (I Wafalm 12: 13-14). Yeroboamu akawatolea wazee wale lugha kali  na ya kunya aliyoshauriwa na vijana wa vijiweni. Baada ya lugha hiyo kukawa na mpasuko mkubwa wa kabila la waisraeli, makabila kumi ya kaskazini dhidi ya makabila mawili ya kusini. “Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo” (IWafalme 12:1-19).  Mpasuko wa mtindo huo ndiyo ulioibuka katika jumuia ya Wakristu wa kwanza.

Yesu akaona asuluhishe shauri hili, akawaita mitume wake na kuwaambia: “Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.” Luka anasema vibaya zaidi kwamba “Wafalme wa Mataifa huwatawala na wenye mamlaka juu yao huitwa wafadhili” (Lk: 22:25), yaani wale wanaowatawala wanajifanya kuwa wafadhili kumbe ni ulaghai na wizi mtupu.

Ndugu zangu, tunaweza kujihoji ni fundisho gani ambalo Marko anataka kulitoa na linamwelekea nani anapowaumbua mitume hawa wawili na wakristu hawa wa jumuia ya kwanza na tukikumbuka Mpasuko wa Taifa la Waisraeli. Mosi, ni kwamba hali hii ya kuwania umaarufu na kutaka kujiweka kimbelembele ni kishawishi kikubwa sana kinachowapata waamini wale ambao ni wa mfano mzuri, wanaowajibika sana katika dini, wanaowasaidia sana wengine, wanaoshirikiana vizuri na wengine, waaaminifu kwa jumuia zao, wenyeviti wanaowajibika sana katika kazi za parokia, wenyeviti waaminifu wa Legio ya Maria, Wana Moyo Mtakatifu wa Yesu Viongozi, wa jumuia ndogondogo bila kuwasahau Makatekista, Watawa bora wa kiume na kike, Mapadre wa mfano na Maaskofu nk. Watu hao ndio wanaoweza kukumbwa na kishawishi cha kujiona wanastahili kukaa kiti cha mbele na kupata nafasi ya kwanza katika mikutano, katika tafrija, nk. 

Kishawishi kinachoweza kukubadilisha fikra bila kujielewa mwenyewe kutoka kwenye hali nzuri ya kuhudumia na kuwajibika kwa wengine hadi kwenye kutaka kuwania kuwa pahali pa pakee. Mungu ameweka hali ya kutaka kuwa wakubwa ndani ya kila mmoja wetu. Hiyo ndiyo hali halisi ya ulimwengu huu. Jaribu pia kufungua macho na kuona hali hiyo katika taifa letu na sababu za mipasuko mbalimbali ndani ya vyama vya siasa, mpasuko wa wananchi walioungana. Chanzo ni Ukuu! Lakini Yesu anataka kuonesha jinsi gani ya kupata ukuu huo.

Ukitaka kuwa wa kwanza uwe mtumishi (Diakonos) wa hiari tofauti na dunos maana yake mtumwa, yaani mtumishi kwa kulazimishwa. Yesu anasema tena: “Anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.” Kuwa mtumishi wa wengine ni mzigo (utukufu) hasahasa kuwa mtumishi wa wote hata wa maadui wako. Tutakuwa huru na wenye furaha kama tunatumikia. Tuzuie mipasuko katika jumuia zetu kwa kutumikiana kwa upendo.

Na Padre Alcuin Nyirenda. OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.