2015-10-04 16:44:00

Tafakari ya Neno la Mungu: Domenika ya XXVII ,Mwaka B.


Ninakusalimu nikikukaribisha katika kipindi chetu cha tafakari Neno la Mungu. Tunaendelea na masomo ya Dominika ya 27 ya mwaka B. Mama Kanisa atushirikisha upendo wa Mungu akitufundisha mpango wa Mungu kuhusu maisha ya ndoa. Ndoa ni kati ya mke na mme wakiwa katika usawa kwa maisha yote pasipo kutengana isipokuwa hutenganishwa na kifo. Mapendo ya mke na mme ni kielelezo cha mapendo yaliyopo kati ya Kristu na mchumba wake Kanisa.

Mpendwa mwana wa Mungu, katika somo la kwanza toka kitabu cha Mwanzo tunaona jinsi Mungu anavyoratibisha kazi yake ya kuumba akisema nitampa Adamu msaidizi wa kufanana naye. Jambo la kwanza tunaloliona ni kwamba Mungu anawaumba mke na mme wakiwa sawa mbele yake. Tokana na hali hiyo aliyoiratibisha Mungu, mke na mme wanapaswa daima kuishi kama wenzi wa ndoa na si mtu na mjakazi wake.

Katika historia ya mwanadamu tamaduni mbalimbali zimeonesha udhaifu mkubwa katika kumtazama mwanamke kama kiumbe dhaifu na hivi kuwa kama chombo cha kutumia katika familia badala ya kuwa mshiriki kamili wa haki na wajibu katika familia. Ndiyo kusema tunaalikwa na Neno la Mungu kufikiri upya na kujaribu kurekebisha mawazo potofu juu ya mwanamke. Tunapaswa kuangalia zaidi juu ya mapendo kati ya wawili na namna ya kuyakuza na si suala la nani mkubwa na nani mdogo.

 

Rafiki yangu mpendwa, katika maisha ya ndoa kuna shughuli mbalimbali za kutenda zikiwa ni pamoja na kuunda umoja kamili yaani kuwa mwili mmoja. Kwa jambo hili Mungu ataka ndoa kuwa ya kudumu na isiyotenganishwa kwa nguvu za kibinadamu. Mke na mme wanapofunga ndoa maana yake wanawajibika kuunda familia ambapo lengo mojawapo ni kuleta maisha mapya duniani, ndiyo kuzaa watoto na kuwalea. Kupendana kwelikweli ni wajibu wa wanandoa hawa, kwa maana hiyo watakuwa wanadhihirisha mapendo kati ya Bwana na Kanisa lake. Kamwe watu wa ndoa baada ya kuunda familia yao hawataingiliwa na wazazi au na awaye yote, hii yataka kuleta uhuru kamili katika kushughulikia mapendo yao na kushika wajibu wao wenyewe vema.

 

Katika somo la pili kutoka katika Barua kwa Waebrania, Mama Kanisa ataka tujifunze juu ya upendo na unyenyekevu wa Mungu yaani, Mungu aliye mkuu anashuka kwa ajili ya ukombozi wetu. Anachukua mwili wa mtumwa ili autakatifuze na kuwa mwili wa utukufu. Anateseka na hivi anashiriki mateso ya mwanadamu ili mwanadamu anayeteseka ashiriki mateso ya Kristu na hivi kwa njia hiyo kuna wokovu. Bwana anaposhiriki ubinadamu wetu atudhirishia pia kuwa yuko pamoja nasi katika maisha ya ndoa na miito mingine. Ndiyo kusema mateso yaliyopo katika ndoa twaweza kuyavumilia kama Bwana alivyovumilia kwa ajili ya wokovu wetu.

 

Mpendwa mwanatafakari, Mwinjili Marko atuletea mafundisho ya Bwana juu ya muunganiko wa kudumu yaani, maisha ya ndoa. Ndoa katika mpango wa Mungu ni ya kudumu na haitenganishwi ingawa tamaduni mbalimbali zinaonesha udhaifu katika kuelewa jambo hili. Basi, Bwana anapoulizwa na Mafarisayo kwa nini Musa aliruhusu talaka, anajibu akisema ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo Mungu alipoumba mme na mke. Kwa hakika aliwaumba na kuwaweka katika maisha ya ndoa yaliyo ya kutegemezana na yaliyo ya kudumu mpaka kufa! Kwa maisha ya ndoa wawili wanawaacha wazazi wao na wanakuwa mwili mmoja na hivi haiwezekani kutenganisha mwili mmoja isipokuwa kupasua na kuondoa ugonjwa fulani au kuponyesha kidonda!

Kumbe tunamwona Bwana akikemea wale wanaoshabikia talaka na anawaaambia wale wote wafanyao hivyo, waunda genge la uzinzi katika maisha yao. Kwa mafundisho ya Bwana tunaalikwa kuwa waamini waliojaa mapendo katika kushiriki miito yetu kikamilifu, tukiongozwa na Roho wa Mungu daima na si vionjo vyetu. Tunapaswa kutambua Mungu anataka daima kulinda utu wa mwanamke na mwanamme katika maisha ya kijamii, ili ule uhuru wa wana wa Mungu ukamilike siku kwa siku mpaka ukamilifu wa dahari.

Basi ninakutakia mapendo daima katika maisha ya ndoa na ukazidi kukomaza ushirika mtakatifu unaomjali mwenzi wako wa ndoa na hasa kuzidisha uaminifu ulio mzizi wa fungamano hilo. Tumsifu Yesu Kristu.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya Cpps

.








All the contents on this site are copyrighted ©.