2015-10-04 16:14:00

Maisha Mchanganyiko: kuishi na wazee


Karibuni nyote katika makala Dunia Mama ambamo tunaendelea kujielimisha na masuala mbalimbali yanayohusiana na maisha mchanganyiko,  tukiwa ndani ya familia ambamo kwa kawaida tuna baba , mama, watoto na wazee na wagonjwa.

Katika wakati huu ambamo Mababa wa Kanisa, wameanza  Mkutano wa Sinodi kwa ajili ya kutazama kwa makini Wito  na Utume wa Familia ndani ya Kanisa na ulimwengu wa Kisasa, leo Kipindi Dunia Mama kinapenda kuanza na kundi la wazee, ambao ni mzizi mkuu wa familia. Wazee wetu tunaoishi nao ndani ya familia na nje ya familia zetu ambao tunakutana nao makanisani na mitaani.  Alhamis iliyopita ambayo ilikuwa ni tarehe Moja Oktoba, dunia iliadhimisha siku ya Kimataifa ya Wazee. Ilikuwa ni Siku nzuri ya kupendeza kwa vijana kuwaenzi watu wenye umri mkubwa  wazee  waliohekimishwa na uzoefu wa maisha. Wanasayansi wanasema kuzeeka ni suala la maendeleo kimaisha na wanafalsafa wanasema uzee ni  chemchemi ya hekima katika maisha ya familia , kijamii na katika mipango ya kiuchumi.

Kumbe basi tunapowazungumzia wazee, tunaoishi  nao katika familia na nje ya  familia zetu ,inapaswa kuwa kwa heshima zote, maana ni stahili yao. Tena tunawaheshimu  kwa ufahamu  kwamba, kuishi kwao miaka mingi kumewapa  uzoefu wa kutosha kimaisha na wameona mengi pia na  hivyo wanakuwa ni hazina kubwa kwa vizazi vipya.

Kwa kujali umuhimu wa kundi hili la  vijana wa juzi , Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe moja Oktoba kuwa Siku ya Kimataifa ya Wazee. Kwa mwaka huu Siku  ya Kimataifa ya wazee, iliadhimishwa chini ya kauli mbiu: Wazee , Nguvu Mpya  ya Maendeleo. Huu ni wito makini, unaopaswa kufanyiwa kazi na lika la vijana , kuona maana yake ni nini hasa.

Mwenye Heri  Papa Paulo VI , katika waraka wake wa Maendeleo ya Watu , akitaza wajibu wa familia alisema , hakuna binadamu anayeweza kusema anajitosheleza mwenyewe kimaisha, bali ameunganishwa na wengine katika mfumo wa kijamii, na hili linamhusu kila mwana familia wa lika zote.  Kumbe hata yule mkongwe asiyejiweza uwepo wake ndani ya familia huleta ujotojoto wa mshikamano na kuwajibika na kiungo hiki asili kinachounganisha binadamu mmoja kwa mwingine.

Sayansi ya maisha ya watu inaonyesha kwamba kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani kote kuhusu maisha ya watu, kwamba dunia ya watu inaendelea kuzeeka zaidi ya kuwa kijana kwa maaana kwamba idadi ya watu wazee inakuwa kubwa kuliko vijana. Takwimu zimetolewa kwamba, duniani kote kuna jumla ya watu millioni 600 wana umri wa miaka zaidi ya 60, idadi inayotazamiwa kuwa mara mbili ifikapo mwaka 2025. Na kwamba hadi mwaka 2050 wazee watakuwa karibia billioni mbili, na wengi wao watakuwa katika nchi zenye viwanda vichache, ambako kwa wakati huu kuna idadi kubwa ya vijana na watoto.  Kumbe kama ilivyonena Kaulimbiu ya adhimisho la Siku ya Kimataifa ya wazee kwa mwaka huu, Wazee , wanaendelea kuwa nguvu mpya ya Maendeleo.

Mpendwa , pengine hapa mtu angeuliza ni umri upi mtu anaweza tajwa katika kundi la wazee ? Wachambuzi wa maisha ya jamii wanasema mtu huingia katika kundi la wazee kuanzia umri wa miaka 65 hadi 74, baada ya umri huo mtu huingia katika kundi la kuitwa mkongwe. 

Umoja wa Mataifa ukitafakari kwa kina mabadiliko haya ya maisha ya watu, unaonya kwamba , kwa kadri dunia inavyozidi  kuzeeka  kwa  haraka, ndivyo mchango wa wazee unavyozidi kuhitajika kupitia kazi za urithishaji  uzoefu na maarifa, licha ya kuwa msaada kwa  familia zao na majukumu. Na hivyo unasisitiza haja ya kuongeza ushiriki wa  wastaafu  katika utendaji wa kazi mbalimbali, kwa  malipo yanayostahili  hata kama ni wana umri wa kustaafu.

 

Tayari  mpaka sasa,  hakuna anayeweza kukanusha kwa jinsi wazee wanavyotoa  mchango wao  mkubwa kwa jamii. Kwa mfano,  Afrika na mahali pengine,  mamilioni ya watu wazima wagonjwa, hasa maradhi yasiyoponyeka haraka kama UKIMWI au saratani , hutuzwa nyumbani na wazazi wao. Na kinapotokea kifo,  watoto yatima wanaoachwa  na wazazi, mara nyingi hubaki katika uangalizi wa bibi au babu.  Takwimu zinaonyesha kwa sasa,  kuna kundi la watoto milioni 14 chini ya umri wa miaka 15 katika nchi za Afrika peke yake, walio chini ya uangalizi wa babu na bibi  zao. Lo ni raha iliyoje kulea wajukuu!
Taarifa mbalimbali zinaonyesha pia kwamba,  si tu katika nchi zinazoendelea ambako wazee wana jukumu kubwa katika maisha na  maendeleo ni muhimu, lakini hata katika nchi za Magharibi , zinazojiita zimeendelea. Mfano unatolewa  nchini Hispania, wanao fanya kazi kubwa ya kutunza  watu binafsi tegemezi  hasa wanaokabiliwa na maradhi mbalimbali ,wagonjwa  wa lika zote,  zaidi hufanywa na  wazee  majumbani  mwao na hasa wanawake wazee.

Mpendwa , Ni matumaini ya kipindi Dunia katika wakati huu wa Sinodi ya Maaskofu juu ya utume wito na utume wa familia ndani ya kanisa na ulimwengu wa Kisasa, kwamba  katika maamuzi yake paia watatoa tamko kwa ajili za kichungaji kwa watu wazee na utume wao katika kanisa. Moja ya nyaraka za Baraza la Kipapa kwa ajili ya Walei, inaeleza kwamba, Maendeleo ya kisayansi, hasa  maendeleo katika uwanja wa tiba na  dawa, umechangia kwa kiasi kubwa katika  miongo ya hivi karibuni, kuongeza muda wa wastani wa maisha ya binadamu. Jina la kizazi cha tatu, limekuwa sehemu kubwa ya idadi ya watu duniani : watu wastaafu katika kazi ya ajira ya kazi, lakini, wanabaki kuwa rasilimali kubwa ndani ya familia , wakiwa na uwezo wa kutoa mchango kwa  manufaa ya familia na umma.

Ni vyema kwamba ,  Mama Kanisa daima huonyesha kujali hali hii ya uwepo wa wazee, na sasa kutokana na taarifa hizi za idadi ya wazee kuwa kubwa kuliko watoto na vijana , Kanisa linapaswa tangu sasa kuandaa utaratibu wa kukabiliana na hali hiyo, mbayo grafu hii ya idadi ya watu inapaswa kuwa kinyume chake.  Tumeona  Ripoti ya mwaka ya  Siku ya Kimataifa ya wazee iliyotolewa na WHO, kwamba idadi ya watu duniani iko katika kasi kuzeeka, kiasi kwamba,  2050, idadi ya watu duniani  walio na umri wa zaidi ya miaka 60 itakuwa mara mbili kutoka asilimia  11% hadi 22%. Hili ni jambo la kutisha, hasa kwa kujiuliza nani atakuwa nguvu kazi ya jamii iwapo sote tunachechemea kwa uzee? 

Watu vijana wanaweza tishika na hali hiyo,  hasa kuwa na uchovu wa kuhudumia wazee. Baba Mtakatifu Francisco akiiona mbali kuzuka kwa tatizo la vijana kuchoka kuhudumia wazee , akihutubia maelfu ya watu,  Jumapili ya tarehe 28 Septemba, ,mwaka jana , alikemea moyo wa kutaka kukatisha maisha ya wazee  aidha kwa huduma mbovu za kutowajali akiita ni   “eutanasia” ya kimyakimya kwa wazee ambayo hufanywa na baadhi ya watu  iwe majumbani au katika taasisi. Papa alisema uwepo wa wazee majumbani, huziba pengo la upweke fulani katika mahusiano ya kifamilia. Papa Francisco alieleza na kutoa mfano wa jinsi Papa Mstaafu Benedikto XV1, ambaye mwaka huu ana miaka 88,  uwepo wake ndani ya Vatican, ambako anaishi kama babu nyumbani kwake, kunaleta faraja na jotojoto la uhai  wa  maisha Vatican.

Tafakari za Baba Mtakatifu Francisco kwa  wazee , zinatongoza katika kuona  thamani ya uwepo wa watu wenye  maisha marefu,  kwamba  huwa na mengi ya kusema katika maisha ya jamii.  Na alitoa wito wa kuheshimu  utu na haki zao msingi . Alihimiza uwajibikaji wa mtu binafsi, familia , vyama, serikali na mashirika ya kimataifa, katika kufanikisha  afya  na huduma bora kwa wazee. Na alionya Wazee wasibaguliwe  au kuhesabika kama  watu waliomaliza muda wao, watu wa kuwekwa pembeni kwanza katika huduma , lakini wao ni sehemu ya jamii hata katika mchakato wa mabadiliko ya maisha, kiuchumi na kiutamaduni.

Katika wakati huu ambamo sote tunaungana na Mababa wa Sinodi  huku tukisubiri kwa hamu matokeo ya sinodi hii juu ya Wito na utume wa familia, tunaitwa pia kuwaombea wazee wetu,  hasa wanaoshiriki katika mchakato huu wa Sinodi , hekima na uzoefu wao , uweze kusikilizwa na wajumbe wa sinodi.  Aidha na tukumbuke wajibu wetu kama sehemu ya familia katika kuhudumiana daima,  tukiwa na wepesi wa kuomba ruksa kabla ya kutenda jambo, kushukuru kwa kila jambo na kuomba samahani kwa mapungufu yetu hata kwa wazee wetu. Basi kwenu nyote kwa wakati huu nawaomba myaandike maneno haya mioyoni mwenu , Naomba, Asante na samahani kuwa ni silaha ya kudumisha umoja na mshikamano wa kila familia na jamii. Daima tukumbuke kusema kwa wazee wetu , Naomba , Asante na Nisamehe.

Makala haya huandaliwa nami TJMhella. 








All the contents on this site are copyrighted ©.