2015-09-25 08:52:00

Papa asikitishwa na janga lililotokea kwa Mahujaji Waislamu Mecca.


(Vatican Radio) Alhamisi , Papa Francisko  alipokea kwa masikitiko habari za janga lililotokea nje kidogo ya mji wa Mecca ambako  watu zaidi ya mia saba, wamefariki dunia na wengine zaidi ya mia nane kujeruhiwa kutokana na kukanyagana wakati wa  sherehe za Siku Kuu ya Eddi el Haji. Waislamu kutoka pande mbalimbali za dunia hukusanyika mjini Mecca kila mwaka,  kwa ajili ya kuadhimisha Siku Kuu ya Iddi el Haji,  katika Madhabahu Matakatifu kwa dini ya Kiislamu “Kaaba" iliyoko Mecca  Saud Arabia.

Papa alitoa salaam za rambirambi, kabla ya homilia yake katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrick la Mjini New York, ambako aliongoza Ibada ya Masifu ya Jioni .Alisema,  “ningependa sana salaam hizi kwa ndugu hawa Waislamu, wake kwa waume ziwe na joto joto la la kisherehe badala ya kuwa za uchungu wa majonzi kutokana na tukio la kutisha lililotokea katika Siku Kuu hii”. Papa alieleza kwa sauti ya majonzi  yenye kuashiria ukaribu wake kwa Waislamu wote, katika uso wa janga hili, lililoutikisa mji wa Makha na aliwahakikishia sala zake na ukaribu wake. .








All the contents on this site are copyrighted ©.