2015-09-21 08:29:00

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA XXV YA MWAKA B, 20Septemba 2015


Tunakuletea ujumbe wa Neno la Mungu, Dominika ya 25 ya mwaka B wa Kanisa. Mama Kanisa anatufundisha wajibu wa Jumuiya kuwakumbatia maskini na walio wahitaji. Katika wimbo wa mwanzo Dominika ya 25, Bwana anasema mimi ni wokovu wa watu, na watu hawa wakinililia nitawaokoa katika taabu zao. Ndivyo basi Jumuiya ya Kikristu inavyopaswa kuwasikiliza na kuwakumbatia walio maskini.

Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Hekima ya Sulemani, na mwandishi anatupa bado sura ya mtumishi mwaminifu ambaye wanajamii wenzake wanamwonea wivu na wanaweka vitisho na vikwazo mbalimbali dhidi yake. Hata hivyo kwa kuwa ni mtumishi mwenye haki, yule aliyemtuma atamlinda mpaka mwisho. Kwa kuvumilia mateso katika upole na unyenyekevu anakuwa mfano kwa watesi wake na jumuiya nzima.  Mtumishi huyu anayetabiliwa na mwandishi wa kitabu cha Hekima anajitokeza katika sura ya Bwana wetu Yesu Kristu katika Agano Jipya.

Mpendwa mwanatafakari, jambo la mateso kwa waliowakweli na watu wa haki katika mazingira ya leo linajitokeza bado na hivi je warudi nyuma au wasonge mbele katika kuvumilia magumu hayo? Kama Bwana wetu Yesu Kristu alivumilia mateso mpaka kufa, basi nasi tuliosafishwa katika Damu yake yatupasa kufuata nyayo zake mpaka mwisho.

Mtume Yakobo anaendela mbele kutufundisha juu ya maisha ya kila siku, leo anatupa Hekima itokayo juu kuwa kielelezo safi cha maisha ya mkristu. Anasema yeyote aifuataye Hekima hiyo atakuwa kinyume na machafuko na fitina katika maisha ya Jumuiya. Machafuko mbalimbali na hasa vita katika ulimwengu wa leo ni matunda ya tamaa za kimwili, na hivi Mt. Yakobo ataka tuzame zaidi katika Hekima ya kimungu itokayo juu, Hekima ambayo hutazama kwa upole na subira mambo yote na hasa kwa njia ya sala inayotangaza mapenzi ya Mungu. Anataka pia sala yetu iwe ni sala iliyojaa imani na tumaini na si tamaa za kimwili.

Katika somo la Injili, Mt Marko anatuonesha Yesu aliye katika utume na wakati huo anatoa katekesi kwa wanafunzi wake. Ni katika katekesi hiyo, Bwana anaendelea kukazia fundisho la kupokea kikombe cha mateso na kisha siku ya tatu kufufuka. Kwa kuwa Mitume bado wana mawazo ya Masiha mwenye nguvu za kivita hawasikilizi vema fundisho hili na badala yake wanajiuliza wao kwa wao, hivi mkubwa ni nani kati yetu! Wanafikiri juu ya vyeo katika ufalme wa Yesu Kristu Masiha! Huu ni udhaifu na hasa waonesha kuwa hawajaelewa kitu!, hawajaelewa Bwana analenga wapi na njia gani anaifuata kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Ni udhaifu unaokuja kwa sababu katika historia ya ulimwengu kulikuwa na matabaka, ambayo mpaka hivi leo yapo tele.

Kwa kuwa Bwana, daima ni mwenye huruma na mvumilivu atatulia na kisha atawafundisha nini maana ya kuwa Mtume, nini maana ya kuwa mkubwa katika Jumuiya, nini maana ya kuwa kiongozi. Ndiyo kusema ukubwa katika Jumuiya ya Kanisa, uongozi ni kutumikia na kuhudumu jumuiya katika mahitaji yake na hasa kutangaza Injili ya Bwana.  Mhudumu anatakiwa kuwapokea wale wote wanaohangaika katika jumuiya, walio kama watoto wadogo. Bwana anaweka picha ya watoto wadogo mbele yetu kwa sababu katika jumuiya ya Kiyahudi mtoto ingawa wanampenda lakini bado anasadikika kutokuwa safi kwa sababu hatunzi sheria na makatazo mbalimbali.

Mpendwa mwanatafakari, katika jumuiya zetu hivi leo, katika nchi zetu jambo la nani mkubwa limeshika kasi kubwa mno kiasi kwamba malumbano ni makubwa mno. Utasikia daima ugomvi kwa sababu ya madaraka katika nchi zetu. Leo basi Neno la Mungu latuambia tuachane na mambo ya kushikilia vyeo kama ndiyo mwisho wa maisha yetu bali kama njia ya kuwatumikia wengine kwa upendo na hekima ya kimungu. Ndiyo kusema kama hatutafanya hivyo tuko nje ya ukristu, tuko nje ya matarajio ya mataifa na jumuiya zilizotuweka katika mamlaka hayo.

Ninakutakia furaha na matumaini katika kushika mafundisho ya Bwana aliye Masiha mteswa lakini mshindi kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.