(Vatican Radio) Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Nchi ya Vatican, Ijumaa (14 Agosti) alisisitiza umuhimu wa kuwepo muungano thabiti kati ya imani na utamaduni mahalia. Kardinali alieleza hilo akiwa katika ziara aliyoianza tarehe 10 Agosti kwanza kwa kutembelea Indonesia na baadaye kwenda Timor ya Mashariki ambako amekuwa kwa muda wa siku tatu kwa ajili ya kilele cha maadhimisho ya kitaifa tarehe 15 Agosti, kwa ajili ya kutimia karne tangu uinjlishaji uanze katika taifa hilo. .
Ijumaa 14 Agosti ,wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshima yake
na Waziri Mkuu Rui Maria de Araujo wa Timor ya Mashariki, Kardinali Parolin, akiongea
kama mwakilishi wa Papa katika maadhimisho ya kutimia karne tano ya Uinjilishaji Timor-Mashariki
na utiaji wa saini katika Mkataba kati ya Jimbo la Papa na Timorya Mashariki , alitoa
shukurani zake za dhati kwa makaribisho mazuri aliyoyapata akiwa katika nchi hii ya
Timor ya Mashariki.
Aliongeza “ ni heshima kubwa kuwa mahali hapa na hasa kama mwalikishi wa Baba Mtakatifu
Francisko, ambaye daima hupenda kukumbusha watu wote, umuhimu wa kuzingatia uadilifu
iwapo, kwa ajili ya kuwa na dunia yenye maisha ya watu yaliyojengwa katika msingi
wa haki , mshikamano na udugu". Na akasema , "Siyo siri, uhusiano ya Jimbo Takatifu
na Timor ya Mashariki una mambo mengi ya kawaida ambamo wanashirikiana kimaadili,
kwa ajili ya kuhakikishia maendeleo muhimu endelevu kwa watu wa Timor. Uhusiano uliosimikwa
katika mzizi wa muungano wa kipekee wa imani na utamaduni wa miaka mingi ambao mwaka
huu kihalali wanasherehekea kupita kwa miaka mia tano tangu kuanzishwa katika taifa
hilo”.
Kardinali Parolin aliendelea kueleza kwamba, ni wazi hawawezi kukanusha ukweli
kwamba muungano huu unaweza tu kuwa endelevu iwapo kila upande utaendelea kudhamiria
kuheshimu majukumu yaliyotajwa katika mkataba juu ya utendaji wa ndani ya serikali,
na ndani ya asasi za kiraia, na ndani ya Kanisa kama wachungaji wa kundi walilopewa.
Na akataja kwamba, historia imeonyesha kwa bahati mbaya, wakati umoja kama huu, unapopuuzwa
au kuchukuliwa kama jambo jepesi, hujengwa mwelekeo wa kuepuka misingi ya maadili
ya imani na utamaduni. Na hivyo mara husababisha kuporomoka kwa haki za msingi za
binadamu, zikipuuzwa na hata kukataliwa.
Katika hali hiyo, Kardinali alisisitiza ni muhimu kwa Mamlaka zote mbili serikali
na Kanisa, kufanya kazi pamoja kwa kuheshimiana na uelewa kwamba wote utumishi wao
ni kwa manufaa ya watu wote, katika hamu yao kwa kutambua maadili yao na matarajio
yao . Na hivyo katika sherehe hizi za kutimia karne tangu Habari njema ya wokovu wa
Kristo kufikishwa Timor ya Mashariki, linakuwa ni tukio muhimu linaloonyesha muungano
thabiti wa imani na utamaduni katika taifa hilo pendwa la Timor ya Mashariki. Na
hiyo ndiyo maana katika maadhimisho ya Jubilee hii ya karne Tano za uinjlishaji pia
imekuwa ni nafasi nzuri ya kuthibitisha kwa mara nyingine uwepo wa ushirikiano kati
ya kanisa Katoliki na serikali, kwa kuweka saini katika Mkataba huu wenye viungo
vya kihistoria, ikilenga kuwahakikishia wote kwamba muungano huu si tu unaendelea
hivihivi lakini kwa uwepo wa hoja ya nguvu ya ushirikiano na mshikamano kwa manufaa
ya watu wote wa Timor wenyewe.
Aidha alitaja kwamba kitendo cha kusaini Mkataba imekuwa ishara kubwa ya kuonekana
katika njia zote za mawasiliano kwa ya manufaa ya jamii na Kanisa. Ni ishara kubwa
inayoonyesha matunda mazuri yalizozaliwa kutokana na mahusiano mazuri kati Kanisa
na Serikali. Na ni hatua muhimu katika hija ya Kanisa Katoliki kwa watu wa Timor
ya Mashariki, walioifanya pamoja kwa miaka mia tano iliyopita. Uhusiano huu ni wa
kipekee, na wenye thamani kubwa kwa Jimbo Takatifu na Timor ya Mashariki, ushirikiano
ulio wazi hata katika Katiba ya Timor ya Mashariki.
All the contents on this site are copyrighted ©. |