2015-07-31 12:21:00

Marekani inasubiri kwa hamu kubwa hotuba ya Papa Francisko kwa Seneti!


Familia ya Mungu nchini Marekani inaendelea kujiandaa kwa ajili ya kumpokea na kumkarimia Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Marekani kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 27 Septemba 2015. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kabisa Baba Mtakatifu anatembelea nchini Marekani. Wengi wanasubiri kusikiliza hotuba ambayo anatarajiwa kuitoa hapo tarehe 24 Septemba 2015 kwenye Congress ya Marekani.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kuhutubia Congress hii. Hadi sasa uongozi wa Congress umepitisha sheria kwa ajili ya kutambua wale watakaoshiriki katika mkutano huo na Baba Mtakatifu Francisko. Taarifa zinaonesha kwamba, Maseneti peke yao ndio watakaohudhuria kutokana na ufinyu wa nafasi na kwamba, hakutakuwa na uwezekano wa kuongeza viti kama ilivyokuwa inatokea kwa wageni mashuhuri wanapohutubia.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo ulinzi na usalama wa kutosha anasema Emily Schillinger, msemaji mkuu wa Rais wa Bunge la Marekani. Kwa wale wote ambao hawatapata nafasi ya kuingia kwenye Ukimbi wa mikutano, kuna Televisheni kubwa ambayo itawekwa nje, ili kuwawezesha wananchi kuangalia kile kinachoendelea ndani ya Bunge.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.