2015-07-30 08:17:00

Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni!


Ndugu yangu! Tunaongozwa katika tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 18 ya Mwaka B wa Kanisa na vifungu vifuatavyo kutoka kwenye Maandiko Matakatifu: Kut. 16:2-4, 12-14, 2. Efe. 4:7, 20-24, 3. Yoh. 6:24-35. Dhamira ya Ekaristi inaendelea kutawala masomo yetu tunaposoma sehemu hii ya Injili ya Yohani sura ya 6. Tunashangaa kuona jinsi mkate huu unavyoshibisha wenye njaa. Ukipokelewa kwa imani, hulisha imani yetu, kwamba anayeshiriki ekaristi takatifu aweza kusema anapata kile alichohitaji. Tunasikia kwa ujumla katika masomo ya leo habari juu ya chakula cha dunia, chakula cha mbingu na baadaye Yesu anaongea kuhusu kumwamini na kumkubali.

Katika somo la kwanza la leo, Mungu anawapa Waisraeli chakula, ila lengo la Mungu ni kuwataka waelewe njaa na kiu ya kumfahamu yeye zaidi, yaani Neno lake. Hapa tunaona kuwa mara baada ya kuwatoa utumwani, wako katika jangwa la Sinai na wanaanza kulalamikia kwanza maji mabaya (Kut. 15:22-27), halafu wanakumbuka vyakula vya huko Misri. Katika hali hii ya malalamiko Mungu anawapatia chakula. Haya ndiyo mazingira yaonekanayo katika somo la kwanza.

Tunafahamu kuwa binadamu anahitaji la aina mbili za chakula, nacho ni cha mwili na chakula cha roho. Ila kadiri ya fundisho la Bwana, chakula cha roho hutangulia na kuwa na maana zaidi. Sehemu hii ya injili tunayosoma leo inafuata mara sehemu ya injili ambayo Yesu alifanya miujiza ya kuongeza mikate. Ila Yesu anawaambia wazi kuwa wanamfuata kwa vile walikula ile mikate wakashiba. Tunakumbushwa na maandiko mfano ktk Mt. 4: 4 – kuwa mtu haishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu. Na katika Yoh. 4:34 – tunasoma – chakula changu ni kutimiza mapenzi ya Baba yangu aliyenituma.

Shida anayokutana nayo Yesu ni uelewa tofauti wa wale watu waliokuwa wanamtafuta. Ndiyo maana Yesu anasisitiza mahangaiko yetu yawe kwa chakula chenye uzima na si kile kiharibikacho. Na anaongea kuhusu lengo hilo la juu kama mkate wa uzima. Alikuwa na maana gani? Kadiri tukatakavyosoma sehemu ifuatayo katika sura hii ya 6 atamaanisha hicho chakula kuwa ni mwili wake mwenyewe na damu yake mwenyewe. Mkate huu hufananishwa na ufunuo toka kwa Baba. Kutoka Kitabu cha nabii Isaya sura ya 55– tunapata nafasi ya kuona jinsi Nabii anavyoongea kuhusu ukuu wa neno la Mungu.

Hata hivyo, wanamwuliza tufanyeje ili tuzifanye kazi za Bwana? Hata baada ya kula mikate na kushiba bado walihitaji ishara zaidi. Na wanamdai Yesu. Ili waamini. Ni kazi gani utafanya? Hata wafuasi walihitaji alama zaidi. Na Yesu anawahakikishia ishara kubwa zaidi kuliko hiyo na kwamba ni Mungu mwenyewe atakayewapa chakula. Naye anawajibu hii ndiyo kazi ya Bwana – kumwamini yeye aliyemtuma. Ni mwaliko kwa watu kumwamini Mungu, yeye atoaye chakula kisichoharibika. Askofu Louis Antonio Tagle anasema kwamba – katika Ekaristi, kanisa linaungana na Yesu katika kumwabudu Mungu wa uzima.

Somo la kwanza laongelea kuhusu chakula cha mwili na bila shaka watu wale waliokuwa na njaa hawakuwa na haja ya chakula cha kiroho kwa wakati ule. Ila Kanisa linatupatia Injili ya leo ili kuweza kuelezea vizuri ukamilifu wa huo mpango wa Mungu. Aidha katika kitabu cha Hekima 16:26 – tunasoma neno hili - ili wanao uliowapenda wajifunze, ee Bwana, kwamba si aina nyingi za matunda zinazomlisha mtu, bali neno lako lawahifadhi wanaokutumainia.

Hata hivyo, ni tabia ya Mungu kuwalisha watu chakula cha mwili na katika kufanya hivyo anawapa nafasi ya kutambua kwa undani hitaji la chakula cha kiroho. Anachotakiwa kutambua mwanadamu ni kuwa roho ya mtu haishibishwi kwa chakula cha mwili, yaani na yote yale yapatikanayo ulimwenguni. Daima inahitaji la kitu kikubwa zaidi ingawa haijui kwa uhakika hicho inachokitamani. Na ndiyo maana kanisa limekuwa likijikita katika huduma za kijamii ili kumwezesha mwanadamu kimwili pia.

Lakini pia katika kufanya hivyo linatoa elimu ili kumwezesha kujua pia yale yapitayo ya kawaida hata kumwezesha kuyaelewa mapenzi yake Mungu. Kumpatia hamu na uwezo wa kujua yaliyo ya juu zaidi. Katika Injili twaona Yesu akialika watu waende kwake, wamwamini, wamtazame, wamsikilize na wajifunze kwake. Baaadaye wale waliomsilikiliza wanajibu na kusema Bwana tupe chakula hicho na jibu la Yesu, mimi ndimi mkate wa uzima, na ajaye kwangu hataona njaa, na aniaminiye hataona kiu tena. Tumshukuru Mungu kwa kutupatia chakula cha uzima wa milele.

Tumsifu Yesu Kristo.

Na Padre Reginald Mrosso. C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.