2015-07-30 07:08:00

Wajibu na dhamana ya wanandoa katika kazi ya uumbaji!


Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya miaka 47 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipochapisha Waraka wa Kitume: “Maisha ya binadamu” “Humanae vitae”, hapo tarehe 25 Julai 1968. Ni waraka wa kinabii unaobainisha kwa kina na mapana dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoshiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kujikita katika maisha na furaha ya wanandoa katika maisha na utume wao ndani ya familia. Papa Paulo VI alikuwa na upeo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu.

Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka huu wa kitume alipembua kanuni maadili na mafundisho ya Mama Kanisa kuhusu mwono na maisha ya mwanadamu tangu pale anapotungwa mimba hadi pale mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Akakazia kwa namna ya pekee wazazi kuwajibika katika kushiriki kazi ya uumbaji, kulea na kutetea zawadi ya maisha, kwa kuheshimu mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kwa njia hii wanandoa wanaweza kuwa kweli waaminifu katika tendo la ndoa na mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kukataa kishawishi cha kukumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vitendo vya utoaji na uzuiaji mimba.

Kanisa linakazia umuhimu wa waamini kuambata kanuni maadili na utu wema; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao kama kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Kanisa linapenda kuwaona waamini wake wakiwa makini kushuhudia Injili Familia inayoambata Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Askofu msaidizi Paolo Martinelli wa Jimbo kuu la Milano katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, Waraka wa Maisha ya Binadamu ni ujumbe wa kinabii unaokabili changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo kuhusiana na Injili ya Familia, Injili ya Uhai, utu na heshima ya binadamu. Mwenyeheri Paulo VI aliona changamoto hizi, akazivalia njuga, kiasi cha kubaki peke yake akikabiliwa na kinzani kutoka ndani na nje ya Kanisa. Aliwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua na kuheshimu Injili ya Uhai kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kichungaji nchini Ufilippini alikazia kwa namna ya pekee Waraka wa kichungaji wa Mwenyeheri Paulo VI kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto za ulimwengu mamboleo. Papa Paulo VI alibaki peke yake kwani alitoa ushuhuda uliokuwa unakinzana na maisha ya watu wa nyakati zake, hali ambayo inaendelea hadi wakati kutokana ukanimungu, mawazo mepesi mepesi na watu kumezwa mno na malimwengu, kiasi cha kutaka kumweka Mwenyezi Mungu mbali na maisha pamoja na vipaumbele vyao.

Askofu msaidizi Paolo Martinelli anakaza kusema, Waraka wa Maisha ya Binadamu unajikita katika mahusiano ya kina kati ya upendo unaopaswa kumwilishwa katika maisha ya ndoa na familia; dhamana na wajibu wa wanandoa kuendeleza, kusimamia na kutetea Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Huu ni mwaliko wa kukata katu katu kukumbatia utamaduni wa kifo unaojielekeza hata wakati mwingine wa kutaka kupata mtoto kwa gharama yoyote ile.

Matokeo yake ni baadhi ya wanawake kugeuzwa kuwa ni maabara ya kuzalisha watoto kwa njia ya chupa! Hapa kuna hatari ya watoto kugeuzwa kama bidhaa inayoweza kupatikana sokoni ikiwa kama mtu ana jeuri ya “vijisenti” vyake. Lakini ikumbukwe kwamba, mtoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni matunda ya upendo kati ya bwana na bibi katika kifungo cha ndoa, kadiri ya Mafundisho ya Kanisa.

Hapa wazazi wanapaswa kuwajibika mbele ya Mungu na jamii inayowazunguka kwa kukazia uhuru katika ukomavu! Hii ndiyo changamoto endelevu inayotolewa na Mwenyeheri Paulo VI. Upendo katika maisha ya ndoa na familia unajikita katika uhuru, wajibu na utashi kamili. Hapa si mambo ya kujisikia tu! Waraka huu anasema Askofu msaidizi Paulo Martinelli haukupokelewa kwa mikono miwili, hali ambayo hata Mwenyeheri Paulo VI alitambua fika kwamba, angekumbana nayo, lakini akasimama kidete kutangaza Injili ya Uhai inayojikita katika utu na heshima ya binadamu kadiri ya mpango wa Mungu.

Papa Paulo VI alionesha dhamana na wajibu wa Kanisa katika kulinda, kutetea na kuendeleza maisha ya mwanadamu bila kuogopa. Binadamu anapaswa kupewa heshima na kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo ya binadamu na kamwe asigeuzwe kuwa ni kichokoo cha tamaa za kibinadamu. Ndoa iwe ni kielelezo cha  hali ya juu kabisa cha upendo wa mwanadamu unaowajibisha, unaopania kuendeleza kazi ya uumbaji kadiri ya mpango wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.