2015-07-30 09:02:00

Msimshabikie Yesu Kristo ili awafanyie miujiza! Awalishe na kuwajaza mapesa!


Wakati fulani katika nchi kunaibuka mtu anayeweza kukonga mioyo ya watu kwa kutoa matumaini makubwa hasa kwa maskini kwa njia ya kuwagawia bure mahitaji muhimu ya maisha yao. Ni dhahiri pia kwamba maskini hao watamshabikia na kumshukuru mfadhili huyo hata kumtaka awe kiongozi wao kwani, “Mkono mtupu haulambwi.”  Lengo la kumshukuru na kumtukuza hivyo ni kumtaka aendelee kuwafadhili. Endapo mfadhili huyo hataendelea kugawa mali, hapo ni dhahiri ushabiki utakoma mara moja na watu wakapotezana maboya na kusambaratika. Hiyo ndiyo ajali inayompata mgawa mali bure kama “mamantilie pangu pakavu”. Ndipo unapojiuliza, “hivi watu hao walimshabikia mtu au mali yake?”

Hali kama hiyo tuliishuhudia katika Injili iliyopita ambapo lukuki ya watu waliohamasika kiasi cha kumtaka Yesu ashike dola kwa vile aliwagawia chakula (mikate na samaki). Yesu akawashtukia, akawapiga chenga ya mwili: “Yesu, akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga akaenda tena mlimani yeye peke yake.”

Wakati Yesu amekwenda mlimani peke yake; nao wanafunzi wakaingia mashuani peke yao wakielekea Kafarnaum; na mkutano umeachwa solemba kama tunavyosoma: “Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu.” (Yoh. 6:24). Watu wanajiuliza, kulikoni msambaratiko huo baada ya ushabiki ule mnene wa majichano yale ya mikate na samaki?

Ndugu zangu, leo tuko ng’ambo ya bahari ndani ya Sinagogi la Kafarnaumu; na kwa dominika tatu mfululizo Yesu atatuhutubia na kutuelewesha maana ya ishara ile ya mikate. Yawezekana lukuki ile ya watu ni wewe na mimi tunaohitaji kueleweshwa maana ya ishara ile ya mikate. Hebu tufuatilie ujumbe anaotupatia Yesu. “Hata walipomwona ng’ambo ya bahari” (kumbuka Wayahudi kuvuka Bahari ya Shamu hadi Jangwani). Kumbe, tukitaka kumwona Kristo yatubidi tuvuke na twende ng’ambo kwenye nchi ya uhuru. Ili kuupata ujumbe wa Yesu aliyeishatutangulia kuvuka ng’ambo, yaani hatuna budi kuondokana na utumwa wa ubinafsi wetu.

Mkutano walipomwona tu Yesu kule ng’ambo wakajidai kumsabahi eti: “Rabi, wewe umeingizana lini hapa?” Ukweli wa mambo walitaka kumwuliza: “Utarudia tena lini lile zoezi la kugawa bure mikate na samaki?” Yesu anawapunguzia uvivu na kuwalipua kimachomacho: “Amin, amin, nawaambieni: Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.” Yesu amewashtukia kumbe, wanatafuta “mamantilie” na hawatafuti Neno litakalowafanya wajenge wenyewe maisha yao. Wanataka kushibisha matumbo! Haki walahi, njaa ni mwana malegeza kweli kweli!

Yawezekana kishawishi cha namna hiyo kinawapata wafuasi wengi wa dini siku ya leo. Mathalani, kule kuvutika zaidi na madhehebu yanayofanya mazingaombwe ya pekee, sala za pekee, vikundi vya ibada za ajabu za uponyaji na zinazovuta huruma ya Mungu! Usishangae wengine wakavutika na miujiza ya kujazwa “mapesa”. Kidhati watu hao hawamfuati Mungu anayetufundisha jinsi ya kuishi maisha yetu, bali wanamshabikia Mungu anayetufanyia miujiza na kutatua matatizo yao, pengine ni matatizo ya mpito!

Kwa hiyo, suala kubwa tunalopishana lugha na Yesu linahusu chakula, yaani Yesu amekuja kutupatia aina gani ya chakula. Yesu mwenyewe anasema: “Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu” (Yoh. 6:27). Katika kigiriki kuna maneno mawili yanayomaanisha uzima au maisha: Kuna Bios maana yake uzima wa kimwili (wa kibaolojia) tuliopewa na wazazi pale tunapozaliwa. Uzima huo unakoma tunapokufa. Halafu Zoé yaani  uzima udumuyo daima zoén ionion, - uzima wa milele. Uzima huu udumuo siyo ule ujao, bali uzima wa sasa unaotolewa na Yesu mwenyewe.

Mungu anatupatia uzima huo tunapozaliwa. “Kwa hiyo hatulegei; ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku…. Tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana, kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.” (II Wakor. 4:16; 18). Uzima wa kimwili (kibaolojia) unachakaa polepole tunapozaliwa, lakini zoé ionion utu wa dani wa unaodumu daima na unakuwa na nguvu zaidi tunapokua. Uzima wa kimwili unalishwa kwa mkate ili uweze kukua na kustawili, kadhali uzima wa Kimungu ulio ndani mwetu hauna budi kulishwa kwa Hekima na Neno la Mungu.

Katika Agano la Kale mkate na maji ni alama ya Hekima au Neno la Mungu, hivyo hulisha na kuchipusha mbegu ya haki na upendo iliyopandwa ndani mwetu ili ikue, izae na kuwagawia wengine matunda ya wema.  Sasa “Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?” ndilo swali walilomwuliza Yesu, yaani Hekima hiyo ya upendo itastawije na kukua ndani mwetu? Swali hilo linaweza kuelekezwa pia kwetu. Sisi tunasali, tunafunga, tunatoa sadaka, tunahudhuria jumuia ndogondogo, tunaenda misa za Jumapili na hata misa za kila siku, tunaimba kwaya, nk.

Matendo kama haya yanaweza kututia kiburi cha kujiaminisha kuwa tunalisha vyema mbegu ya uzima (zoé)  iliyopandwa ndani mwetu. Sasa tunajiuliza “zaidi ya hapa tufanye nini?” Yesu anajibu kifupi tu: “Mwaminini Yeye aliyetumwa na Yeye.” Kuanzia sasa tutalisikia neno hili “kuamini.” Neno hilo halina maana ya imani, bali ni kuunganisha kabisa maisha yako na ya Yesu Mnazareti ili uwe kama yeye mwenye uzima wa milele.

Mkutano wakaendelea kumdadisi maswali “Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? Baba zetu waliila mana jangwani kama ilivyoandikwa, Akawapa chakula cha mbinguni ili wale.” Mashaka haya nayo ni mazito na ni fundisho kwetu. Kwa swali hili umati unaonesha waziwazi kuwa unataka kupata upendeleo wa pekee katika kumfuata Yesu kama walivyopendelewa Wayahudi walipogawiwa bure mana jangwani. Kasoro hiyo ipo kwa Wakristo wa leo. Waamini tunapenda kujiaminisha kwa Yesu ili tupate upendeleo na fursa ya pekee.

Kumbe, ampendaye Yesu inatosha aunganishe maisha yake na ya Yesu kwa sababu nafsi ya Yesu peke yake  ni muujiza, ndiyo maana anasema: “Amin, amin, nawaambieni: Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu ndiye anayewapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.” Chakula hicho kilichoshuka toka mbinguni ni Yesu Kristo mwenyewe. Ndiyo maana tunasali: “Utupe leo mkate wetu wa kila siku.”

Mkate huo si kitu kingine isipokuwa ni Yesu Kristo mwenyewe. Yesu anahitimisha: “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.” Kauli hii ya Yesu ni nzito na haijawahi kutamkwa na yeyote katika hitoria ya binadamu. Kadhalika ni kauli itakayomgharimu sana Yesu kuyatolea maelezo na kumsababishia kunung’unikiwa (kumkataa, kumdharau) na mfarakano kati ya wafuasi. Ama kweli hivi ndivyo ilivyo kwa wapendanao hasa kwa anayempenda Mungu: “Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai, lini nitakapokuja nionekane mbele ya Mungu?” (Zab. 42:2). Mkate pekee unaoshibisha maisha, ni Neno la Yesu, hususani nafsi yake. Ukimwelewa utaaminisha maisha yako kwake na kumpenda kwa dhati.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.