2015-07-30 07:36:00

Mchakato wa upatanisho, haki na amani nchini Uganda


Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, hivi karibuni ilifanya semina iliyowashirikisha wajumbe kutoka katika majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini Uganda ili kushirikishana uzoefu, fursa, changamoto na matatizo yanayojitokeza katika mchakato wa upatanisho, haki na amani; mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu Barani Afrika.

Wajumbe katika semina hii, wameangalia kwa kina na mapana mahusiano yalipo kati ya: Upatanisho na Uponyaji; ukweli, haki na amani; umuhimu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika mchakato wa upatanisho pamoja na dhamana na wajibu wa waamini walei katika harakati za upatanisho kama kielelezo cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Upatanisho, haki na amani ni cheche za maendeleo endelevu kwa nchi ambayo inataka kudumisha mafao na ustawi wa wananchi wake, kwani kinzani, migogoro na vita ni mambo yanayokwamisha maendeleo ya watu kiroho na kimwili. Wananchi wa Uganda wanayafahamu haya kwa kina na mapana.

Mchakato wa upatanisho unapania pamoja na mambo mengine kujenga na kudumisha mahusiano mema kati ya watu, jamii na serikali, kwa kujikita katika kanuni maadili, ukweli na uwazi ili kuanza mchakato wa uponyaji wa kitaifa, kutokana na wananchi wengi wa Uganda kuathirika na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imedumu kwa miaka kadhaa.

Monsinyo John Baptisa Kauta, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, amewataka wajumbe kuambata neema na baraka za Mwenyezi Mungu katika maisha na utume wao, ili kukoleza mchakato wa upatanisho wa kitaifa nchini Uganda. Hapa watu wanapaswa kuonesha moyo wa toba na wongofu wa ndani, tayari kutoa na kupokea msamaha. Watambue kwamba, neema na baraka ya Mwenyezi Mungu itawasaidia kusonga mbele, ili kujenga na kuimaarisha upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa. Umoja ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa waja wake na kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake.

Kanisa Katoliki nchini Uganda limeendelea kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa upatanisho kati ya Serikali ya Uganda na Kikundi cha Waasi wa Uganda, “Uganda Resistance Army” ambacho kimekuwa ni mwiba mkubwa dhidi ya haki, amani na maendeleo ya wananchi wanaoishi Kaskazini mwa Uganda. Watu wengi wamepoteza maisha yao, wametekwa nyara na kubakwa; wamelazimika kuyakimbia makazi yao na zaidi ya waganda millioni mbili hawana makazi ya kudumu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda katika barua yake ya kichungaji ya mwaka 2004 lilikazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Ili kufikia lengo hili, Serikali na Kikundi cha Waas inchini Uganda walikuwa wanalazimika kuweka silaha chini na kuanza mchakato wa upatanisho. Juhudi hizi ziliungwa pia mkono kunako mwaka 2007 wakati Umoja wa Wakristo nchini Uganda ulipoanzisha mchakato wa majadiliano na upatanisho Kaskazini mwa Uganda.

Miaka miwili baadaye, Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na Baraza la Majadiliano ya kidini nchini Uganda waliitisha mkutano wa pamoja ili kujadili mustakabali wa taifa la Uganda kwa kujikita katika misingi ya haki, amani. Mkutano huu ulihudhuriwa na wadau mbali mbali. Hadi leo hii, wananchi wengi wa Uganda wana kiu ya kuona haki, amani na upatanisho wa kweli vinatawala kama kikolezo cha maendeleo endelevu ya watu: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.