2015-07-30 07:55:00

Matumizi ya chupa za plastik yanachangia uharibifu mkubwa wa mazingira


Mtandao wa maji kiekumene, EWN ambao uko chini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, hivi karibuni umeanzisha kampeni ya kimataifa ya kutaka kupiga rufuku matumizi ya chupa za plastiki katika biashara ya maji, kwani chupa hizi zinachafua mazingira na kusababisha hatari kubwa kwa maisha ya viumbe hao na kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inapitisha azimio litakalofanya maji kuwa ni haki msingi za binadamu.

Haya ni kati ya mambo msingi yaliyopitishwa katika mkutano wa mtandao huu uliokuwa unafanyika huko Geneva, Uswiss. Wajumbe wanakiri kwamba, kuna madhara makubwa ya kiafya yanayotokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa kutokana na mchakato wa uzalishaji hadi matumizi ya chupa za plastiki katika biashara ya maji.

Chupa za plastiki ambazo zilipaswa kutumika tena, lakini sehemu kubwa ya shehena za chupa inaishia kuwa ni taka zinazoendelea kutupwa na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wengi duniani. Kuna mamillioni ya tani za chupa ambazo ziko baharini, kwenye maziwa na mito. Chupa hizi kamwe hazitaoza na zitaendelea kuwa ni sehemu ya kero na uchafuzi wa mazingira. Hapa kuna haja kwa Serikali kuhakikisha kwamba zinafanya maboresho ya mitandao ya maji, ili kuhakikisha kwamba, wananchi wao wanakua na maji safi na salama katika makazi yao.

Katika nchi zilizoendelea zaidi duniani, matumizi ya maji ya chupa za plastiki ni makubwa kutokana na kampeni kubwa zinazofanywa na makampuni yanayozalisha bidhaa ya maji kwa kuwaaminisha kwamba, kwa kunywa maji ya chupa wana uhakika wa maisha na usalama wao, ikilinganishwa na maji yanayotoka moja kwa moja kwenye bomba.

Wajumbe wa mtandao wa maji kiekumene wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchapisha Waraka wa kitume juu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Wanasema, Baba Mtakatifu amegusia masuala msingi yanayopaswa kuzingatiwa kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Amekazia umuhimu wa maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo yake; athari za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha kwa kuonesha mshikamano zaidi.

Kampeni ya Kwaresima inayofanyika katika kipindi cha majuma sita, kwa mwaka 2016 itazinduliwa nchini Palestina, kama sehemu ya hija ya haki na amani mjini Yerusalem. Kampeni hii inajikita katika dhana ya haki ya maji, kama sehemu ya maandalizi pia ya mkutano juu ya mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika nchini Misri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.