2015-07-29 15:27:00

Mwanadamu si mmiliki wa mazingira, anapaswa kuyalinda na kuyatunza!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini katika barua yake ya kichungaji kwa Familia ya Mungu nchini humo kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote linakaza kusema hii ni changamoto na wajibu wa haki jamii. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira mintarafu mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mwezi Desemba 2015, huko Paris, Ufaransa. Hapa kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linawaalika kwa namna ya pekee kabisa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Binadamu anapaswa kutambua kwamba, amepewa dhamana ya kulinda na kutunza na wala si mmiliki wa mazingira. Dhana hii inawezekana, ikiwa kila mtu kadiri ya nafasi na dhamana yake atawajibika kikamilifu.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini kwamba mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mjini Paris, utatoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi, kwa kuweka kando masilahi binafsi ambayo yameendelea kukwamisha juhudi za kutunza mazingira nyumba ya wote na waathirika wakubwa ni maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi!

Haki jamii, mafao ya wengi na maendeleo endelevu ni vigezo msingi katika sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote, kwa ajili ya watu wa kizazi hiki na kila kijacho! Maendeleo endelevu hayana budi kujikita katika mshikamano wa kimataifa na ustawi wa dunia nzima. Dunia ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu ili aweze kutawala na kuiendeleza. Maendeleo na mshikamano ni mambo msingi katika utekelezaji wa haki jamii wanasema Maaskofu Katoliki Ufilippini.

Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapotafakari kuhusu mafao ya wengi, dhana hii iwasaidie pia wanasiasa na watunga sera na sheria kumwilisha mawazo haya katika uhalisia wa maisha ya watu mahalia. Ikiwa kama sera na mikakati ya maendeleo haitao kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na utunzaji bora wa mazingira, watu wengi wataendelea kuathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu katoliki Ufilippini limekamilisha ujenzi wa makazi 132 yatakayokabidhiwa kwa waathirika wa tufani ya Yolanda iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kanisa limekabidhi makazi haya tarehe 29 Julai 2015 baada ya kubarikiwa. Hiki ni kijiji cha upendo ambacho ujenzi wake umechangiwa na wasamaria mbali mbali walioguswa na mahangaiko ya wananchi wa Ufilippini wakaamua kuwaunga mkono, kielelezo cha mshikamano wa upendo na utandawazi unaojali shida na mahangaiko ya watu.

Kanisa Katoliki nchini Ufilippini limekwisha changia kiasi cha Euro millioni 9. 7 kwa ajili ya shughuli za ukarabati na ujenzi wa makazi ya watu walioathirika kutoka na tufani ya Yolanda iliyotokea kunako mwaka 2013. Watu zaidi ya millioni kumi na moja waliathirika. Ili watu waweze kurejea tena katika hali yao ya kawaida kunahitajika walau kiasi cha dolla billioni nane.

Hadi sasa takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu 1, 700 ambao hawajulikani walipo kutokana na majanga yaliyosababishwa na tufani ya Yolanda. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linapokazia umuhimu wa kutunza mazingira kama nyumba ya wote linatambua madhara na hasara zake, kwani tufani ya Yolanda, iliwagusa na kuwatikisa, ikaacha mamillioni ya watu wakiogelea katika umaskini, magonjwa na mahangaiko ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.