2015-07-29 14:53:00

Mchango wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika kukuza majadiliano na Wayahudi


Onesho la picha za Mtakatifu Yohane Paulo II na Waamini wa dini ya Kiyahudi linalofanyika mjini Vatican; onesho limezinduliwa siku ya Jumanne, tarehe 28 Julai 2015 mjini Roma. Ni onesho la picha za Yohane Paulo wa pili tangu wakati wa ujana wake hadi alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Onesho hili linatarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe 17 Septemba 2015. Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza onesho kama hili lilifanyika kunako mwaka 2005 kwenye Chuo kikuu cha Mtakatifu Xavier, Cincinnati, Marekani. Onesho linaloendelea mjini Vatican ni sehemu ya kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Nostra aetate, Waraka wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican kuhusiana na majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali dunian.

Tukio hili limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali kutoka ndani na nje ya Vatican. Dr. James Buchanan kutoka Chuo kikuu cha Xavier, Marekani anasema, onesho hili ni kielelezo cha majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi kadiri ya mtazamo wa Mtakatifu Yohane Paulo II na viongozi mbali mbali wa dini ya Kiyahudi. Ni Onesho linalojikita katika mahusiano yanayofumbata cheche za uchungu na mahangaiko ya ndani; mwaliko wa toba, wongofu na kukuza majadiliano ya kidini.

Kwa upande wake Dr. William Madges kutoka Chuo kikuu cha St. Joseph, Philadelphia, Marekani anasema, onesho hili ni kielelezo cha baraka kwa waamini wa dini hizi mbili. Ni wazo lililoibuliwa wakati wa kumbu kumbu ya miaka 85 ya kuzaliwa kwa Papa Yohane Paulo II. Tukio hili lilikuwa na changamoto nyingi lakini kutokana na ushirikiano wa pande mbali mbali, likazinduliwa na kuwa ni daeaja la urafiki wa dini hizi mbili. Lengo la onesho hili ni kuelimisha, kukumbuka na kuhamasisha watu kuona matukio mbali mbali yaliyotendwa na Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kama kielelezo cha majadiliano ya kidini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, ili kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.