2015-07-29 14:40:00

Majadiliano ya kidini hayana budi kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu


Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa linalohamasisha umoja miongoni mwa Wakristo anasema, Jubilei ya miaka 50 ya Waraka wa kitume wa majadiliano ya kidini, “Nostra aetate”, iwe ni fursa kwa waamini wa dini mbali mbali kupiga hatua kubwa zaidi kwa kuboresha mahusiano yanayojikita katika uhalisia wa maisha, kwani maneno matupu hayavunji mfupa. Waamini wa dini ya Kiyahudi na Wakristo wanao urithi mkubwa unaopaswa kufanyiwa kazi kama ilivyojidhihirisha katika mkutano Baraza kuu la Wayahudi na Wakristo uliohitimishwa hivi karibuni mjini Roma.

Waamini wa dini mbali mbali wanaweza kushirikiana na kushirikishana mengi kuhusu haki na amani; mikakati na shughuli na huduma za kijamii pamoja na matendo ya huruma; urithi mkubwa katika maisha ya Wakristo na Wayahudi. Argentina ni mfano wa kuigwa kwani Wayahudi na Wakristo kwa pamoja kunako mwaka 2004 walikusanya fedha na kugharimia miradi iliyopania kuwasaidia maskini, licha ya Argentina kwa wakati huo kukabiliwa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Waathirika wakuu wa mipasuko ya kijamii ni maskini na wote wanaoendelea kusukumizwa pembezoni mwa jamii anasema Kardinali Kurt Koch. Wajumbe katika mkutano ule, walikwenda kujionea hali halisi na kushiriki katika kuwahudumia maskini, kielelezo cha imani katika matendo. Kumbe, kuna uwezekano mkubwa wa kushirikiana kati ya waamini wa dini mbali mbali katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato kwa kuwaonjesha jirani imani inayomwilishwa katika matendo.

Waamini wawe na macho ya kuona na kuguswa na mahitaji ya watoto yatima, wagonjwa, wajane, wazee na maskini katika mazingira yao. Hili ni kundi ambalo kadiri ya Maandiko Matakatifu linapaswa kushughulikiwa kwa upendo mkuu. Miaka hamsini ya “Nostra aetate ni fursa makini ya kutambua mahusiano makubwa yaliyopo kati ya Wayahudi na Wakristo, ili kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Waamini wajifunze kuwa kweli ni majirani, marafiki na wenza katika hija ya maisha ya kiroho na kamwe si adui kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.