2015-07-28 10:58:00

Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika: 29 Julai 2015 - 29 Julai 2016


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM tarehe 29 Julai 2015 linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 46 tangu lilipoanzishwa kunako mwaka 1969, Kampala, Uganda wakati wa hija ya kitume ya Mwenyeheri Paulo VI Barani Afrika. Lengo lilikuwa ni kuliwezesha Kanisa Barani Afrika kushikamana kwa pamoja katika kukuza na kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaojikita katika mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Hii itakuwa pia ni siku maalum ya kuzindua Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika, tukio litakalofanyika wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Sekretarieti kuu ya SECAM iliyoko mjini Accra, Ghana. Maadhimisho haya yatahitimishwa rasmi tarehe 29 Julai 2016, wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa kumi na saba wa SECAM unaotarajiwa kufanyika nchini Angola.

Maadhimisho haya ni sehemu ya mapendekezo yaliyotolewa na Baba wa Sinodi maalum ya Maaskofu wa Bara la Afrika iliyojikita katika misingi ya haki, Amani na upatanisho. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Africae munus, akaitaka Familia ya Mungu Barani Afrika kuwa na siku maalum ya kuadhimisha tukio hili Barani Afrika.

Ni kipindi cha kuomba na kutoa msamaha; kuganga na kuponya madonda ya chuki na kinzani; mambo ambayo yamekuwa ni kikwazo kikubwa cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Afrika. Huu ni mwaka wa Jubilei ya haki, amani na upatanisho, ambamo Familia ya Mungu Barani Afrika inamwomba Roho Mtakatifu asaidie mchakato wa maridhiano na mfungamano wa kijamii Barani Afrika.

SECAM inayataka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Maaskofu mahalia kuwa na ratiba pamoja na mikakati ya maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika, ambao kimsingi unakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani na baadaye Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Matukio yote haya yawasaidie waamini kukua na kukomaa kwa kukimbilia neema, rehema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza upya mchakato wa maisha unaomwambata Kristo na Kanisa lake.

SECAM pia inawaalika Maaskofu kukusanya mchango kwa ajili ya kuitegemeza, ili hatimaye, iweze kutekeleza dhamana na majukumu yake kwa ajili ya Familia ya Mungu Barani Afrika. Mchango huu utasaidia harakati za Uinjilishaji Barani Afrika, ukuzaji wa mawasiliano pamoja na kugharimia shughuli za SECAM. Asilimia 75% ya fedha zote zitakazokusanywa itatumwa kwenye Makao makuu ya SECAM na asilimia 25% ya fedha yote itabaki kwenye mfuko wa Mabaraza ya Maaskofu. Waamini Barani Afrika wanahamasishwa kulienzi na kulitegemeza Kanisa, kwani wafadhili huko N’gambo, wako hoi bin taabani kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na changamoto mbali mbali zinazowakumba! Waamini waoneshe jeuri kwamba, wanaweza kulitegemeza Kanisa Barani Afrika kwa kuchangia rasilimali watu, vitu na fedha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.