2015-07-27 09:05:00

Njia za mawasiliano ya jamii zisaidie mchakato wa Uinjilishaji ndani ya familia


Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, Jumapili tarehe 26 Julai 2015 limeadhimisha Siku ya 49 ya Upashanaji Habari Kitaifa kwa kuvitaka vyombo vya mawasiliano ya jamii kutumika katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Vyombo vya mawasiliano ya jamii viwe ni madaraja ya watu kukutana na kusaidiana na kwamba, wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanawafunda watoto wao matumizi bora ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili waweze kuwajibika barabara, vinginevyo wanaweza kugeuka kuwa kama “kichwa cha mwendawazimu” mahali ambapo kila mtu anafanyia mazoezi.

Askofu Martin Mtumbuka, Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi katika ujumbe wa Baraza unaofanya rejea kutoka katika ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, wanasema, familia ni msingi wa watu kukutana na kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo. Malawi ni kati ya nchi chache za Kiafrika ambayo inaendelea kucharuka katika matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari kwa haraka zaidi.

Mitandao ya kijamii, imekuwa ni sehemu ya maisha ya wananchi wa Malawi mijini na vijijini. Lakini matumizi mabaya ya vyombo hivi vya mawasiliano ya kijamii ni chanzo cha kinzani, migogoro na utengano katika maisha ya ndoa na familia. Wanafamilia wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuliko hata wanavyotumia kwa mawasiliano ya kawaida ndani ya familia. Mambo haya yana madhara yake katika mshikamano na mfungamano wa kifamilia. Baadhi ya vijana wa kizazi kipya wamejikuta wakitumbukia katika mitandao ya picha chafu, mambo ambayo ni hatari kwa ustawi wa maisha yao kiroho na kimwili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, linawageuzia kibao hata Mapadre ambao wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii, kiasi hata cha kushindwa kutoa muda wa kutosha kwa ajili ya maandalizi ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Wanakuwa na muda mchache wa kuzungumza na Mapadre wenzao na matokeo yake, mahusiano ya kijumuiya yanalegalega na hapo unaweza kuwa ni mwanzo wa kumezwa na malimwengu, ikiwa kama Wakleri hawatakuwa makini.

Maaskofu wanajiuliza swali la msingi, ikiwa kama Wakleri waliojitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Kanisa wanamezwa na malimwengu kiasi hiki, Je, wanawezaje kuzisaidia familia kuwa na matumizi sahihi ya njia za mawasiliano ya kijamii, kwa kuwajibika zaidi? Maaskofu wanakaza kusema, familia zinapaswa kuwa ni mahali muafaka pa kukutana na Mwenyezi Mungu. Hii ni shule ya haki, amani, upendo, mshikamano na utakatifu wa maisha.

Hapa wanafamilia wanajifunza kupenda na kupendwa; kusamehe na kusamehewa; kila mtu akitambua karama na mapungufu yake; tayari kuwapokea na kuwakubali wengine jinsi walivyo! Familia za Kikristo zijifunze kuwa na matumizi bora zaidi ya mitandao ya kijamii kwa kukuza na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili; kwa kuweza kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu na kwamba, familia zijenge utamaduni wa kuwasiliana wao kwa wao pamoja na kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu, ili kweli aweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao hapa duniani. Hapa toba na wongofu wa ndani ni mambo muhimu sana katika maisha ya Kikristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.