2015-07-26 13:32:00

Vijana wa zamani! Saidieni kufunda familia tunu bora za maisha na imani!


Wazee wana wajibu na dhamana kubwa ya kuwaimarisha ndugu na jamaa zao katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo sanjari na kuwasaidia watu wao kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu ambaye kamwe hawezi kuwatupa waja wake wanaomkimbilia kwa moyo wa imani na matumaini. Hekima, ujuzi na mapendo ya wazee yasaidie mchakato wa malezi na familia. Ni changamoto na ujumbe unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wazee nchini Hispania, katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Kitaifa inayofanyika Jumapili tarehe 26 Julai 2015 kwa kumbu kumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria.

Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano na uwepo wake wa karibu kwa wote wanaoshiriki katika maadhimisho haya, hususan kwa kutoa huduma makini kwa wazee na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; huku wakichangia ustawi na mafao ya wengi. Siku ya Wazee kitaifa nchini Hispania inahamasishwa kwa namna ya pekee na Chama cha Kitume cha “Edad Dorada- Menajeros de la paz”. Wanachama wa chama hiki wako mstari wa mbele katika kuwahudumia wazee nchini Hispania.

Lengo ni kuendelea kuihamasisha jamii kuwalinda, kuwatetea na kuwatunza wazee sanjari na kuthamini mchango wao katika ustawi na maendeleo ya familia. Jimbo kuu la Madrid ndilo mwenyeji wa maadhimisho haya kwa mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.