2015-07-25 15:15:00

Waonjesheni wengine huruma ya Mungu inayokoa na kuponya!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Tunapoelekea kuuzindua Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu hapo tarehe 8.12.2015, tuajiandae vema kwa kusali na kuendelea kuuchambua Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Misericordiae vultus yaani uso wa huruma. Ndani ya waraka huu, Baba Mtakatifu anabainisha mpango mkakati wa kulifanya Kanisa liwe kweli chombo cha wokovu wa mwandamu. Anatualika sote kuelewa nafasi na wajibu wetu katika kuchangia kuleta wokovu huo.

Kwa msisitizo mkubwa zaidi,  Baba Mtakatifu tena na tena, amelialika Kanisa kurudi katika misingi, yaani kuihubiri na kuiishi huruma ya Mungu, huku akitualika sisi waamini wote na watu wote wenye mapenzi mema, kuiambata huruma kama vile baba yetu wa mbinguni alivyo na huruma. Ni kwa njia hiyo tutaweza kuimwilisha huruma ya Mungu kwa matendo yale ya huruma ya kiroho na kimwili. Anasisitiza tena na tena Baba Mtakatifu Fransisko, tufumbue macho kutazama, kuona huruma na kuguswa kimatendo na mahangaiko ya jirani zetu.

Anaendelea kusema, katika Injili ya Luka, tunapata kielelezo kingine kitakachotusaidia kuiishi Jubilei yetu kwa imani. Luka anatuambia kwamba, Yesu siku ya Sabato alirudi Nazareti, na kadiri ilivyokuwa dasturi yake, aliingia  katika Sinagogi. Humo walimwita ili kusoma Maandiko Matakatifu na kuyatolea ufafanuzi. Sehemu ya andiko alilolisoma lilitoka katika Kitabu cha Nabii Isaya asemapo “ Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta, ili kuwatangazia Maskini Habari njema, amenituma kuwaganga waliopondeka moyo, kuwatangazia uhuru mateka, na kuwaweka huru waliosetwa; na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa (Is 61:1-2).

Huo Mwaka wa Bwana uliokubaliwa; au mwaka wa Huruma: ndio haswa Mwaka uliotangazwa na Bwana na ndio tunaotamani kuuishi sasa. Mwaka huo utatuletea utajiri wa utume wa Yesu kama ulivyosemwa na Nabii: yaani kuleta maneno na matendo ya faraja kwa masikini; kutangaza uhuru kwa wale waliofungwa katika mifumo mipyaya utumwa katika jamii zetu za kisasa; kuwasaidia vipofu wapate kuona tena hali halisi ya ulimwengu huu, hasa wale walijifungia ndani mwao wenyewe, na kuwarudishia hadhi na thamani wale ambao wamepokwa thamani ya utu wao kama binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Mafundisho haya ya Yesu kwa mara nyingine tena yanapaswa kudhihirishwa katika maisha ya Wakristo ambapo kwa imani wanapaswa kuyaishi katika uhalisia. Na anasema tuyaishi mafundisho hayo huku tukisindikizwa na maneno ua Mtume Paulo asemapo “Yeye atendaye matendo ya huruma, na afanye hivyo kwa ukarimu” (rej. Rum. 12:8).

Kipindi cha Kwaresma katika wmaka wa Jubilei, kitumike kwa umakini zaidi kama wakati maalumu kwa kuadhimisha na kuonja huruma ya Mungu. Ni vipengele vingapi  vya maandiko matakatifu vinafaa kwa tafakari katika majuma hayo ya Kwaresma, ili kutusaidia kuvumbua uso wa Huruwa wa Baba! Tunaweza kuyarudia maneno ya Nabii Mika na kuyafanya kuwa yetu sisi wenyewe; asemapo “Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema.  Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari” (rej. 7:18-19).

Vifungu vya Kitabu cha Nabii Isaya vyaweza pia kutafakariwa kikamilifu wakati wa kipindi hicho cha kusali, kufunga na kutenda matendo ya upendo. Nabii Isaya anasema, “Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?  

Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.  Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;  na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.  (Is. 58:6-11).

Zaidi tena ndani ya Misericordiae vultus yaani uso wa huruma; mintarafu kipindi cha Kwaresma Baba Mtakatifu anaagiza “Masaa 24 kwa ajili ya Bwana, yanayopaswa kuadhimishwa Ijumaa na Jumamosi inayotangulia Dominika ya 4 ya Kwaresma, lazima itekelezwe katika kila Jimbo”. Watu wengi (na hasa vijana pia) huijongea Sakramenti ya Upatanisho; na kwa mang’amuzi hayo wanaivumbua upya njia ya kumrudia Bwana, huku wakiishi katika hali ya sala nyoofu na hivyo kuyapa maana zaidi maisha yao.

Anasisitiza zaidi Baba Mtakatifu “Kwa mara nyingine tena, na tuiweke Sakramenti ya Upatanisho kama kiini cha Maisha yetu, na hiyo itawasaidia watu kugusa ukuu wa Huruma ya Mungu kwa mikono yao wenyewe. Na kwa kila anayetubu, Sakramenti ya Upatanisho itakuwa kwake ni chemchemi ya amani ya kweli moyoni”.

Akiwaelekea mapadre waungamishaji Baba Mtakatifu Fransisko anasema, “Sitachoka kuwasisitiza waungamishi wawe ishara  halisi ya huruma ya  Baba. Hatuwi waungamishi wazuri hivihivi tu. Tunakuwa waungamishi wazuri endapo kwanza kabisa tunajiruhusu sisi wenyewe kuwa waungamaji tunaoitafuta huruma yake kuu.  Tusisahau kwamba, kuwa waungamishi maana yake ni kushiriki katika utume wa Yesu mwenyewe wa kuwa Ishara wazi ya upendo wa daima wa kimungu, upendo wenye kusamehe na kuokoa.

Sisi Mapadre tumepokea Kipawa cha Roho Mtakatifu  kwa ajili ya mandoleo ya dhambi na tunawajibika kwa hilo. Hakuna kati yetu anayestahili nguvu hii, ila tu, tu watumishi waaminifu wa huruma ya Mungu kwa njia ya nguvu hii.  Kila Muungamishi  anapaswa kumpokea muungamaji kama Baba mwema anayeelezewa katika mfano wa mwana mpotevu: baba anayetoka nje, na anakimbia kwenda kukutana na mwanaye, hata kama alikosa kwa kutapanya urithi wake”.

Bado akiwaelekea waungamishi Baba Mtakatifu anakaza kusema “ Waungamishi wanaalikwa kumkumbatia mdhambi anayerudi nyumbani kwa baba, na waoneshe furaha ya kuwa naye tena”. Waungamishi, anasema Baba Mtakatifu “tusichoke kumwendea hata yule mwana mwingine anayesimama nje, asiyeweza kufurahia kurudi kwa mwana mwenzie”. Tumwendee huyo pia na tumwambie hukumu yake juu ya mwenzake ni kubwa mno, siyo ya haki na haina maana mbele ya huruma ya baba isiyona mipaka.

Bado, anaendelea kusisitiza Baba Mtakatifu “katika kiti cha Kitubio, waungamishi wasiwe wanauliza maswali-maswa yasiyo na maana, wawe kama baba mwenye huruma katika mfano ule; aliyeikatikiza litania ya maelezo aliyoiandaa yule mwana mpotevu”. Ni kwa njia hiyo waungamishaji watajifunza kupokea kilio cha msaada na toba kinachotoka katika moyo wa muungamaji. Kwa kifupi, anasema tena Baba Mtakatitu “waungamishi wameitwa kuwa ishara ya ukuu wa huruma ya Mungu daima na popote na katika hali zote, hata iweje”!

Mpendwa msikilizaji, tazama milango ya wokovu ipo wazi kabisa mbele yako. Baba Mtakatifu kwa mafundisho haya anafungua zaidi na zaidi, mwanya kwa kila mmoja wetu kuweza kuchora huruma, wema na upendo wa Mungu vinavyobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kazi ni kwako na kwangu, tuchote neema hizo kutoka katika chemchemi ya huruma ya Mungu inayowaokoa watu wote. Tusikizane tena kipindi kijacho.

Kutoka katika studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.