Kardinali Donald Wuerl wa Jimbo Kuu la Washington, kwa huzuni ametangaza kifo cha Kardinali William Wakefield Baum, kilichotokea siku ya Ijumaa 24 Julai 2015 huko Washington
Akitangaza kifo hiki, Kardinali Wuerl, amekiri huzuni yake kubwa ya kuondokewa na mchungaji huyu shupavu katika utumishi wa Kanisa, lakini pia akasema, anamshukuru Mungu kwa huduma yake, hasa kama Askofu Mkuu wa Jimbo la Washington, alilolitumikia kwa kipindi kirefu. Na kwamba , wema, fadhila na kujitolea kwake katika kuhudumia wito wake kwa Mungu kamwe hazitafuta katika mioyo ya watu. Daima alikuwa ni mtu aliyejazwa na furaha ya kipadre katika kuiishi ahadi yake ya kumtumikia Bwana aliyemwita, katika kazi hiyo, aliyoifanya kwa uaminifu kwa miaka 64 ya maisha yake ya Kipadre. Pia atakumbukwa, mpaka sasa kuwa Kardinali aliyetumikia kwa miaka mingi kuliko Makardinali wote , katika historia ya Baraza la Maaskofu Katoliki la Marekani.
Kardinali Donald Wuerl wa Washington, ameungana na familia ya Marehemu, marafiki na waamini wote wa jimbo la Washington, kuomba kwa ajili yake, huruma ya Mungu, na pia kumtolea Mungu shukurani , kwa ukarimu na utulivu wa Marehemu Baum ambaye huduma yake iliweza kugusa mioyo ya wengi katika kipindi chote cha utumishi wake wa miaka mingi.
Marehemu alizaliwa katika mji wa Dallas (USA), Novemba 21, 1926. Wazazi wake walihamia akiwa bado mtoto, Kansas City, Missouri, ambako alipata elimu ya msingi katika shule ya Parokia ya Mtakatifu Petro McKay.
Mwaka 1939 aliingia seminari madogo ya Mtakatifu John ya Kansas City, aliendelea masomo yake katika falsafa na teolojia katika Seminari Kenrick, St Louis na kupadrishwa Mei 12, 1951.
Baada ya Upadrisho kwa miaka kadhaa alifanya utume wake kama Paroko msaidizi katika Parokia ya Parokia ya Mtakatifu Aloysius ya Jiji la Kansas , pia akiwa mwalimu wa theolojia na historia ya kanisa katika Chuo cha Mtakatifu Theresa. Mwaka 1956 yeye alitumwa na askofu wake Roma, kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu hadi kujipatia shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Angelicum mwaka 1958.
Baada ya masomo alirudi Marekani ambako aliendelea na utume jimboni mwake, Kansas City. Na kutokana na mapenzi yake katika kujenga umoja wa Wakristo,aliingia kama mtaalam mshauri katika kazi ya Mtaguso Mkuu wa II. Pia alishiriki katika mikutano kadhaa kama Mjumbe wa Tume ya Pamoja ya mikutano ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Kanisa Katoliki kuwa Katibu Mtendaji tangu 1964-1967 wa Kamati ya Kiekuemeni ya Mambo ya Ndani ya Mkutano wa Kitaifa wa Maaskofu Katoliki ya Marekani(NCCB) . Katika kipindi hicho, pia jimboni mwake alikuwa Paroko wa Kanisa la Mtakatifu James.
Februari 18, 1970 Papa Paul VI alimteua kuwa Askofu wa Springfield-Cape Girardeau;
naaliwekwa wakfu wa Askofu Aprili 6 ya mwaka huo. Machi 5, 1973, aliteuliwa Askofu
Mkuu wa Washington. Wakati huo huo alikuwa pia Rais wa Tume ya Kiekumeni kwa Mambo
ya Ndani ya Baraza la Maaskofu Katoliki la Marekani.
Papa Yohana Paulo II, alimteua kujaza nafasi ya Mkuu wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili
ya Elimu Katoliki tangu Januari 15 1980 hadi 6 Aprili 1990 alipoteuliwa kuwa Mkuu
wa Mahakama ya Kitume ya Kitubio, kazi aliyo ifanya hadi Novemba 22, 2001. Na alitangazwa
katika orodha ya Makardinali katika kikao cha Makardinali cha a Mei 24, 1976, na kuwa
Askofu wa Jina wa Parokia ya S. Croce, iliyoko mtaa wa Flaminia, jiji Roma.
Kwa kifo cha Kardinali William Wakefield Baum, idadi ya Makardinali Imebaki 220, ambao wenye haki ya kupiga kura ni 120 na wasiokuwa na haki ya kupiga kura imebaki 100.
Sasa tumwombee apate nafasi katika nyumba ya Baba yetu Mbinguni, apumzike kwa amani.
All the contents on this site are copyrighted ©. |