2015-07-22 09:26:00

Rais Uhuru Kenyatta: Vipaumbele: maendeleo, ulinzi na usalama!


Rais Barack Obama wa Marekani anatembelea Kenya kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Julai 2015. Pamoja na mambo mengine, Rais Obama anatarajiwa kushiriki mkutano wa tisa wa kimataifa wa wajasiriamali, utakaozungumzia kuhusu vitega uchumi. Huu ni mkutano unaowashirikisha viongozi, wafanyabiashara, mashirika ya kimataifa na viongozi wa Serikali. Huu ni mkutano unaofanyika walau kila mwaka, tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 2009.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akizungumza na waandishi wa habari Siku ya Jumanne, tarehe 21 Julai 2015 anakaza kusema, Rais Obama atakapokuwa nchini Kenya atakutana na kuzungumza na viongozi wote wa Serikali ya Kenya. Vipaumbele vya mazungumzo ya Serikali ya Kenya na Rais Obama ni maendeleo na usalama wa wananchi wa Kenya. Serikali inataka kujifunga kibwebwe kupambana na baa la umaskini; inataka kuboresha sekta ya elimu, afya na kuendeleza ustawi wa watu wake.

Ulinzi na usalama ni kati ya masuala nyeti ambayo Serikali ya Kenya inataka kuzungumza na Rais Obama wa Marekani. Hii inatokana na ukweli kwamba, katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi, Serikali ya Kenya imekuwa ikishirikiana na kwa karibu zaidi na vyombo vya usalama kutoka Marekani. Mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab yanatishia amani na usalama wa wananchi na mali zao.

Rais Obama akiwa nchini Kenya atafungua mkutano wa tisa wa wajasiriamali, atazungumza na Rais Uhuru Kenyatta; atatembelea kumbu kumbu ya mahali palipokuwa ni Ubalozi wa Marekani nchini Kenya, uliolipuliwa na bomu kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika kunako mwaka 1998. Rais Obama atazungumza pia na viongozi wa vyama vya upinzani na vyama vya kiraia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.