2015-07-21 08:03:00

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini Nigeria!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kwa sasa linaendelea na maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa, itakayoanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 5 Agosti mjini Benin. Tukio hili litazinduliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria.

Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja atatoa mahubiri katika Ibada hii ya misa takatifu inayotarajiwa kuwakusanya vijana wengi kutoka sehemu mbali mbali za Nigeria, licha ya wasi wasi na mashaka ya mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea bado kuitesa Nigeria, licha ya sera na mikakati ya ulinzi na usalama inayofanywa na Serikali iliyochaguliwa hivi karibuni. Viongozi wa utume wa Vijana watashiriki kutoa neno na changamaoto kwa vijana.

Ratiba ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini Nigeria inaonesha kwamba, imesheheni utajiri mkubwa unaoambata kwa namna ya pekee: katekesi makini kwa vijana, sala na tafakari ya Neno la Mungu; shuhuda na majadiliano yanayolenga kubadilishana uzoefu na mang’amuzi ya maisha; mkesha wa sala na tafakari. Askofu Emmanuel Badejo wa Jimbo Katoliki la Oyo anatarajiwa kuwashirikisha vijana kuhusu utandawazi usioguswa na mahangaiko ya watu; vijana kama wakala wa mabadiliko.

Askofu Gofrey Onah wa Jimbo Katoliki Nsukka atafanya tafakari kuhusu Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu, kwa kujikita katika heri wenye huruma maana hao watapata huruma; tema ambayo pia itaongoza maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, Poland. Kwa sasa nchini Nigeria, Msalaba wa Vijana unaendelea kutembezwa kwenye Parokia na taasisi mbali mbali; hija ambayo ilianzishwa kunako mwaka 2014 na itahitimishwa mwishoni mwa mwezi Julai, huko Mjini Benin.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.