2015-07-20 10:18:00

Matendo ya huruma ndicho kipimo cha hukumu yetu siku ya mwisho!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Tunakusalimu kutoka katika Studio hizi za Radio Vatican, Tumsifu  Yesu Kristo! Tunendelee kujumuika katika kuuchambua waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko Misericordie vultus, yaani Uso wa huruma, maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu katika kipindi kilichopita alisema, Kanisa katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu linaalikwa kurudi kwenye misingi. Na mmoja ya misingi hiyo ni kuhubiri na kuiishi huruma ‘kama Baba wa Mbinguni alivyo na huruma’. Na hivyo kila mwamini anaalikwa kwa kina na mapana kuuambata mwaliko huu, kuishi kwa kuimwilisha huruma kiroho na kimwili, na kuitandaza huruma hiyo  kwa watu wote na haswa wale ambao wamesukumizwa pembezoni mwa jamii kama vile, masikini, wakimbizi, wagonjwa, wapweke, wafungwa, wenye njaa, wenye kiu, walioonewa na watu wengine wote kama hao.

Tukiwatazama hao kwa jicho la huruma, na kuwaelekezea mkono wa faraja yenye kujali, huku tukitambua na kuheshimu sana thamani ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; ni hapo tu tutakuwa tunaimwilisha huruma ya Mungu.

Mpendwa msikilizaji, tutakumbuka kwamba, katika kipindi kilichopita tulihitimisha kwa kumsikia Baba Mtakatifu akikazia kwamba, katika mwaka huo wa huruma ya Mungu, tutahitaji kujibidisha sana katika kuyamwilisha matendo ya huruma ya kimwili na kiroho. Na hivyo kila mmoja wetu anaalikwa kwa kweli kufumbua macho kutazama, kutafakari na kutekeleza hayo matendo ya huruma.

Hakika, familia ya mwanadamu inayoumia na kuteseka kwa wakati huu, itakombolewa katika maumivu hayo kwa njia ya kuimwilisha huruma ya Mungu tu; kwa njia ya  hayo matendo ya huruma ya kiroho na kimwili. Na kuyamwilisha matendo hayo kupo katika ngazi zote, kuanzia ngazi ya mtu binafsi, familia, makanisa na vikundi vyote vya watu, ngazi ya kitaifa na kimataifa. Tushikane mikono, tuunganishe mioyo na nguvu zetu tuyaishi matendo huruma kwa maneno na matendo.

Baba Mtakatifu anaendelea kusisitiza kwamba, hatuwezi kuyakwepa maneno yale ya Kristo ambayo yatakuwa kipimo cha hukumu yetu ya siku ya mwisho: Tutaulizwa kama tuliwalisha wenye njaa au tuliwapa maji wenye kiu; tutaulizwa kama tuliwakaribisha wageni au tukawavika walio uchi; Tutaulizwa kama  tulitumia muda wetu kuwatazama wagonjwa na wale walio kifungoni (rej. Mt. 25:31-45).

Na zaidi tutaulizwa kama tuliwasaidia wenzetu kushinda mashaka ambayo yanawapelekea kukata tamaa na kuingia katika hali ya upweke mkubwa; tutaulizwa kama  tumesaidiaje katika kutokomeza ujinga ambao binadamu wengi wanaogelea; tutaulizwa namna gani tumesaidia kuwanusuru watoto kutoka katika vifungo vya ujinga na umasikini.

Tutaulizwa pia kama tumekuwa karibu na wapweke na walioonewa; tutaulizwa kama tuliwasamehe wale waliotukosea; tutaulizwa kama tulijizuia na kukwepa kila aina ya chuki na hasira ambayo hutupeleka katika fujo na machafuko. Tutaulizwa pia kama tumekuwa na uvumilivu kwa wenzetu kama vile sisi wenyewe tunavyovumiliwa na Mungu. Tutaulizwa pia kama tuliwaombea ndugu zetu mbalimbali.

Baba Mtakatifu anasema ‘katika wote hao walio wadogo’ Kristo mwenyewe yupo. Mwili wake unadhihirika katika mwili wa wanaoteswa, wanaodhulumiwa, wanaonyanyaswa na wanaotengwa. Hao wote wanahitaji kutazamwa na kutunzwa na sisi tunaomsadiki Kristo, na binadamu wote, kwani sote tu watoto wa Baba mmoja ambaye ni Mungu. Baba Mtakatifu anahitimisha sehemu hii kwa kutualika tusiyasahau maneno ya Mt. Yohane Msalaba aliyesema “tunapojiandaa kuuacha ulimwengu huu, tutahukumiwa kwa kigezo cha Upendo”.

Kutoka Studio za Radio Vatican mimi ni Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.